21 Oktoba 2022 - 16:45
Guterres ataka walimwengu wabadili mtindo wa maisha na kuishi kwa kutunza mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewatolea mwito walimwengu kwa kuwataka wabadili mtindo wa maisha yao na kuishi kwa kutunza mazingira.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliyeko ziarani nchini India amesema hayo wakati akizindua mpango wa Mitindo wa Maisha unaojali utunzaji wa Mazingira na kuhimiza watu wote kubadili mitindo yao ya maisha na kuishi maisha ambayo yanazingatia si tu kulinda mazingira bali pia kujali kizazi cha sasa na cha baadae.

Guterres amesema kuwa, wakati huu ambapo dunia inakabiliwa na changamoto nyingini wakati mwafaka wa kuweka msisitizo katika kuitunza sayari dunia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, “Hakuna changamoto kubwa inayokabili dunia kwa sasa zaidi ya mabadiliko ya tabianchi, lakini mpango huu wa mitindo ya Maisha kwa kuzingatia mazingira umetengenezwa ili kuangazia ukweli muhimu wa kuleta matumaini ya ukweli, sisi sote tukiwa kama watu binafsi na jamii tunaweza na ni lazima tuwe sehemu ya suluhisho la kulinda sayari yetu na mustakabili wetu wa pamoja.” 

Aidha amebainisha kwamba, mitindo ya maisha ya sasa inaongeza pengo kubwa la utofauti kati ya mtu na mtu huku akieleza changamoto nyingine ni utoaji wa hewa ambayo inaathiri zaidi mataifa masikini ikilinganishwa na mataifa tajiri duniani.

Kadhalika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaja namna ya kupunguza uharibifu wa mazingira na kuishi kwa mitindo mipya ya maisha kwamba ni pamoja na kuokoa nishati na kupunguza uchafuzi wa mazingira na utupaji taka.

342/