Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Ukht. Maysarah Ally, Katika Darsa lake ameeleza na kubainisha kuwa: Katika Uislamu, Mwanamke anaheshimiwa kwa nafasi yake ya kipekee katika jamii. Mojawapo ya nafasi tukufu anayopewa ni ile ya kuwa mama. Uislamu unamtambua mama si tu kama mlezi wa familia, bali pia kama nguzo ya maadili, huruma, na malezi bora ya kijamii.
1_Hadhi ya Mama katika Uislamu
Qur’an na Hadith nyingi zimeinua daraja la mama: Allah anasema: “Na tumemuusia Mwanadamu (kuwafanyia wema) wazazi wake; mama yake amembeba kwa udhaifu juu ya udhaifu...” (Luqman 31:14)
Mtume Muhammad (SAWW) alisema: “Mwenye haki zaidi ya kuandamwa na wema wako ni mama yako.”
Hii inaonesha kuwa Uislamu unamchukulia mama kama chombo cha huruma, uvumilivu na msingi wa maadili ya mtoto.
2_Mama kama Kielelezo cha Upendo
Upendo wa mama wa Kiislamu hauishii kwa mtoto wake tu, bali unaenea kwa familia nzima na jamii kwa ujumla.
Mama wa Kiislamu hujitahidi kutekeleza majukumu yake kwa uaminifu, huruma, na hekima, akilea kizazi kinachoogopa Mungu na kutenda haki.
3_Majukumu ya Mama wa Kiislamu
Malezi ya Kiimani: Mama ndiye mlezi wa kwanza wa mtoto; humfundisha maadili ya Kiislamu, Qur'an, na Sala.
Kuimarisha Familia: Mama ni kiungo muhimu katika kudumisha upendo, mshikamano, na utulivu wa familia.
Kuwa Mshauri: Mara nyingi mama hutoa ushauri wenye busara kwa watoto na mume wake, akisaidia familia kuchukua maamuzi yenye hekima.
3_Changamoto Anazokumbana Nazo Mama wa Kiislamu
a) Majukumu mengi ya kifamilia na kijamii wakati mwingine huambatana na changamoto za kiuchumi na kijamii.
b) Kukabiliana na mitazamo hasi ya kijinsia katika baadhi ya jamii.
c) Hata hivyo, Uislamu unampa heshima na haki zake, na kumpa nafasi ya kusimama kwa haki yake.
4_Mchango Wake kwa Jamii
Mama mwema ni shule bora. Naam, kwa hakika "Mama mwema ni shule bora, ukimwandaa vyema, umeandaa taifa zima."
Wanawake wa Kiislamu kama mama wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika kuimarisha jamii kupitia malezi bora, elimu, na msaada wa kijamii.
Mwisho:
Mama wa Kiislamu si tu mlezi wa watoto bali ni msingi wa jamii yenye maadili.Uislamu umempa heshima ya kipekee kwa nafasi yake, ukimtukuza kama kielelezo cha upendo, subira, na hekima.Kwa hivyo, ni wajibu wa jamii kumheshimu Mwanamke, kumsaidia Mwanamke, na kumpa nafasi ya kutimiza jukumu lake kikamilifu.
Ukth. Maysarah Ally
08 Juni, 2025
Your Comment