Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA), Askofu Dkt. Isreal Maasa Ole Gabriel (wa tatu kutoka kushoto), ameongoza kikao muhimu kilichowakutanisha viongozi wa kitaifa na wadau wa masuala ya diplomasia ya ndani na nje ya nchi. Mkutano huo umefanyika katika ofisi za KM, Golden Rose, Jijini Arusha.
Katika Kikao hicho, viongozi walijadili masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha mshikamano wa kitaifa, kuendeleza juhudi za maridhiano kati ya makundi tofauti ya kijamii na kidini, pamoja na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika masuala ya Amani na Mshikamano wa Kimataifa.
Miongoni mwa washiriki wa kikao hicho ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Nje na Mahusiano ya Kimataifa (IMNMK), Eng. Dkt. Athuman R. Mfutakamba (wa pili kutoka kulia), ambaye alisisitiza umuhimu wa kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia wa Amani na Maridhiano kati ya Tanzania na Mataifa mengine, hasa katika nyanja za ushirikiano wa kijamii na kiuchumi.
Askofu Prof. Rejoice Ndalima (wa kwanza kulia), naye alisisitiza nafasi ya taasisi za kidini katika kuhamasisha maadili mema, Ushirikiano na Mshikamano wa Kitaifa. Aidha, aliwataka viongozi wa kijamii na kidini kuungana ili kupunguza migawanyiko na kuondoa maneno ya chuki miongoni mwa Wananchi.
Kikao hicho kilimalizika kwa makubaliano ya pamoja ya kuandaa mikakati madhubuti ya kitaifa kwa mwaka 2025–2026, ikiwemo mipango ya kufanikisha warsha, semina, na mikutano ya wadau kutoka ndani na nje ya nchi ili kushirikiana katika ajenda ya kudumisha Amani, Maridhiano na Mshikamano wa Tanzania.
Your Comment