Rais Pezeshkian ameyasema hayo alipohutubia hadhara ya wasomi wa Mkoa wa Tehran na kusisitiza kwamba: "haikubaliki kwamba uweke vikwazo kisha useme, hupaswi kuwa na makombora au silaha, na kisha uzungumzie juu ya kufanya mazungumzo mengine tena".
Pezeshkian amesema, mazungumzo lazima yafanyike kwa kuheshimiana, na akasisitiza kwamba Iran haitakubali kamwe kuburuzwa na kufikia makubaliano kwa sababu tu ya kufanya mazungumzo.
Ameeleza bayana kwamba: “wakija kwa heshima, tutajadiliana, lakini hatutakubali kulazimishwa... tangu awali, tulishatangaza kwamba tunataka majadiliano na mazungumzo, lakini si kwa gharama yoyote”.
Itakumbukwa kuwa Rais wa Marekani Donald Trump ambaye alijitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mwaka 2018, yaliyosainiwa na Iran na mataifa mengine kadhaa ikiwemo Marekani yenyewe na kuidhinishwa pia na Umoja wa Mataifa , mapema mwezi huu alirejesha tena utekelezaji wa kampeni yake ya "mashinikizo ya juu kabisa" dhidi ya Iran huku akisema yuko tayari kufikia makubaliano na Iran.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelitolea mjibizo hilo kwa kusema: "anadhani akija na kututisha, kesho tutarudi nyuma na kusema, 'sawa, tunakubali chochote unachosema.' Sisi ni binadamu wenye hadhi. Wakija kwa heshima, tutajadiliana, lakini hatutakubali kulazimishwa".
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Dk. Pezeshkian ameashiria jinai za utawala ghasibu wa Israel huko Ghaza na Lebanon na akasema: "hakuna dhamiri iliyo hai itakayokubali hatua zinazochukuliwa na Israel mtenda jinai dhidi ya watu wasio na ulinzi huko Ghaza, Lebanon na Palestina kwa ujumla."
Ameongeza kuwa, Marekani na Ulaya hazikuunga mkono tu "ukatili" wa utawala wa Israel bali ziliupatia pia utawala huo mabomu na silaha.
Rais Pezeshkian amekumbusha kwa kusema: "laiti kama Waislamu bilioni moja katika eneo wangekuwa wameungana kama ndugu, utawala wa Kizayuni mfanya mauaji ya kimbari wenye idadi ya watu milioni mbili, usingeweza kuwasababishia Waislamu hali kama hii".../
342/
