Gazeti la Yedioth Ahronoth limemnukuu Agam Berger, mwanajeshi wa kike wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambaye alikuwa akishikiliwa mateka huko Ghaza na akaachiwa huru hivi karibuni kupitia mchakato wa makubaliano ya kubadilishana mateka, akizungumzia jinsi wanamapambano wa Brigedi za al-Qassam walivyoamiliana na mateka wa Israel.
Berger amesema, kwa muda wote walipowashikilia mateka, wanamuqawama wa al-Qassam Brigedi walikuwa wakiwapelekea mateka hao Waisrael vitabu vya kidini vya Kiyahudi, ambavyo viliwawezesha kutekeleza ibada za dini yao ya Uyahudi.
Mateka huyo wa Kizayuni aliyeachiliwa, ameashiria jinsi mateka wengine wa Kizayuni walivyostaajabishwa na hatua hiyo na akasema, "hatujui vipi hilo lilitokea, lakini walituletea baadhi ya vitu, ikiwa ni pamoja na kitabu cha maombi; na hili halikujiri kwa sadfa, bali lilitokea wakati tulipokuwa tukivihitaji vitu hivyo".
Mateka huyo Muisrael ameongezea kwa kusema: "mimi mwenyewe na wenzangu tuliokuwa pamoja, tulikuwa tukifuatilia tarehe kupitia redio na televisheni, ambayo ilitusaidia kutambua siku za sikukuu za Kiyahudi wakati tulipokuwa tukishikiliwa mateka".
Berger alikamatwa mateka na vikosi vya Muqawama katika operesheni ya Oktoba 7, 2023, akiwa kwenye kambi ya kijeshi ya kitongoji cha Nahal Oz, na akaachiliwa Januari 30 katika zoezi la kubadilishana mateka wa Kizayuni na Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza ya utawala haramu wa Israel.../
342/
