21 Februari 2025 - 18:05
Ripoti ya Human Rights Watch yafichua jinai ya kutisha ya Israel

Shirika la haki za binadamu la Humar Rights Watch limetoa ripoti mpya inayoonesha ukatili na jinai kubwa ya kuchupa mipaka iliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye Ukanda wa Ghaza.

Shirika hilo limetoa ripoti ya kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel, wanandoa wazee wa Kipalestina katika kitongoji cha Al-Zaytoun kusini mashariki mwa Jiji la Ghaza mwezi Mei mwaka jana. Baadaye wanandoa hao walitumiwa kama ngao ya kivita ya kuwinda raia wengine.

Katika uchunguzi wake kuhusu uhalifu huo, Human Rights Watch na timu ya wanasheria imetaja majina ya wahanga hao wawili kuwa ni Mohammad Fahmi Abu Hussein (aliyekuwa na umri wa miaka 70) na mkewe Mazyouna Hassan Fares Abu Hussein (aliyekuwa na umri wa miaka 65).

Ripoti hiyo Human Rights Watch inasema: "Baada ya kupitia uchunguzi uliofanywa na tovuti moja ya Israel tumegundua kuwa, afisa mmoja wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni kutoka kikosi cha Nahal alifunga mnyororo wa miripuko shingoni mwa mzee huyo Mpalestina na kumlazimisha kuingia kwenye nyumba moja baada ya nyingine katika kitongoji cha Al-Zaytoun ili kuzikagua na kuhakikisha zilikuwa tupu kwa muda wa masaa manane na baada ya kumpa mateso hayo makali, walimpiga risasi na kumuua yeye na mkewe." Uchunguzi wa shirika hilo la kimataifa la haki za binadamu umefichua kwamba, uhalifu huowa kutisha ni pamoja na taarifa zilizopo kwamba wanandoa hao wawili wazee wa Kipalestina, hawakuuawa kwa kupigwa risasi, bali waliuawa kwa mripuko wa myororo huo wa mabomu waliovishwa na wanajeshi makatili wa Israel. Ushahidi wa hayo ni kwamba miili ya Wapalestina hao ilionekana imeripuka vipande vipande na hakuna chochote kikubwa kilichobaki.

342/