5 Machi 2025 - 22:41
Source: Parstoday
Mpango wa Umoja wa Nchi za Kiarabu kuhusu Palestina unapingana na matakwa ya Marekani na Utawala wa Kizayuni

Viongozi wa nchi za Kiarabu, katika mkutano wao mjini Cairo, wamepinga mipango na njama za kishetani za Marekani na utawala wa Kizayuni kwa kukataa hatua za kulazimisha uhamishaji wa Wapalestina.

Jumanne, Machi 4, mji mkuu wa Misri, Cairo, ulikuwa mwenyeji wa mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za Kiarabu uliolenga kujadili matukio ya hivi karibuni kuhusu suala la Palestina na kufikia uamuzi wa pamoja wa Kiarabu kuhusu Ukanda Gaza.

Viongozi wa Kiarabu walioshiriki katika mkutano huo, hususan Misri na Jordan, walisisitiza uungaji mkono wao kwa mpango wa ujenzi upya wa Ukanda wa Gaza na kupinga kurejea kwa vita na uhamishaji wa Wapalestina kwa nguvu.

Katika mkutano huo, viongozi wa Kiarabu walipitisha mpango wa dola bilioni 53 kwa ajili ya ujenzi upya wa Gaza. Mpango huu ni kinyume na mpango wa Rais wa Marekani, Donald Trump, wa "kuchukua usimamizi wa Gaza" na kuwahamisha kwa nguvu zaidi ya Wapalestina milioni mbili.

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Nchi za Kiarabu ulifanyika huku viongozi wa makundi ya Muqawama wa Kipalestina wakitoa wito kwa nchi za eneo kuiunga mkono Palestina. Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, katika taarifa yake, imepongeza msimamo wa mataifa ya Kiarabu wa kupinga juhudi za kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina au kufuta suala la kitaifa la Palestina kwa kisingizio chochote. Hamas ilitaja msimamo huu kuwa wa heshima na ujumbe wa kihistoria.

Katika taarifa hiyo, Hamas pia imesisitiza kuwa Wapalestina, wakiwa na uungaji mkono wa msimamo wa pamoja wa mataifa ya Kiarabu, wana uwezo wa kufelisha njama na mipango hii. Chama cha Ukombozi wa Palestina (PFLP) pia kimekaribisha tamko la mwisho la mkutano wa Cairo na kusisitiza haja ya utekelezaji wa haraka wa maamuzi yake, ikiwa ni pamoja na kusitisha mashambulizi yote na kuanza mara moja kwa ujenzi wa Gaza bila kuingiliwa na mataifa ya kigeni.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu, Ahmed Aboul Gheit, ameeleza kuwa lengo la mkutano wa viongozi wa Kiarabu ni kukataa uhamishaji wowote wa Wapalestina, iwe ni wa hiari au wa kulazimishwa. Ameongeza kuwa mpango wa mataifa ya Kiarabu unataka kuundwa kwa kamati ya kusimamia Gaza kwa muda wa miezi sita. Pia amesisitiza kuwa mpango wa nchi za Kiarabu unaweza kuendelea kubadilika kulingana na matukio mapya.

Katika tamko la mwisho la mkutano huo, Umoja wa Nchi za Kiarabu umetoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupeleka vikosi vya kimataifa vya kulinda amani katika Ukingo wa Magharibi na Gaza.

Mkutano wa Cairo umefanyika wakati ambapo utawala wa Kizayuni unaendelea na vitendo vyake vya kuchochea mivutano, kukiuka mchakato wa usitishaji mapigano na kupuuza maombi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pamoja na taasisi zake ya kusaidia Gaza. Utawala wa Kizayuni unaendelea kuizingira Gaza na kuzuia misaada ya kibinadamu kuingia katika eneo hilo.

Donald Trump, katika mpango wake wa udanganyifu na muovu, ametaka kuanzisha mfumo wa Marekani huko Gaza kwa kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina kwenda mataifa mengine ya Kiarabu na kisha kuimiliki Gaza. Mpango huu umepingwa vikali duniani kote, ikiwa ni pamoja na mataifa ya Ulaya.

Mkutano wa Cairo umeonyesha kuwa viongozi wa Kiarabu wamesimama kwa umoja kupinga hatua za Trump na wanasisitiza haki halali ya Wapalestina kurejea katika ardhi yao.

Suala jingine muhimu lililosisitizwa na viongozi wa Umoja wa Kiarabu ni hitaji la kukomesha haraka uvamizi wa utawala wa Kizayuni huko Gaza. Viongozi wa Kiarabu katika mpango wao wamesisitiza juu ya ujenzi wa Gaza bila kuingiliwa na Marekani.

Mkutano wa Cairo umekuwa ishara ya mshikamano na msimamo wa pamoja wa ulimwengu wa Kiislamu kuhusu mustakabali wa Palestina. Miongoni mwa mada muhimu zilizojadiliwa ni maamuzi ya Wapalestina juu ya utawala wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, pamoja na msaada wa kifedha kwa ujenzi wa Gaza.

Mkutano huo pia umeonyesha ukweli kwamba viongozi wa Kiarabu, kwa kuzingatia historia ya utawala wa Kizayuni ya uvamizi na msaada wa mara kwa mara kutoka serikali ya Marekani, wanataka kukomesha hali hii na kuzingatia mahitaji halali ya watu wa Palestina.

Mabadiliko ya kieneo baada ya usitishaji mapigano kati ya utawala wa Kizayuni na Hamas yanaonyesha uzingatiaji mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu na viongozi wa Kiarabu kwa matakwa halali ya Wapalestina. Historia ya mzozo wa Palestina inaonesha kuwa utulivu na usalama katika eneo hilo utapatikana na kudumu pale tu njama za utawala wa Kizayuni na washirika wake katika Ikulu ya Marekani zitakabiliwa kwa uzito unaofaa.

Kwa ajili ya kuimarisha utulivu na amani katika eneo, ni muhimu kuvunja mipango hatari na yenye kuvuruga amani ya Marekani na Kizayuni, ikiwa ni pamoja na uhamishaji wa lazima wa Wapalestina kutoka Gaza na, kwa upande mwingine, kukomesha uvamizi wa Kizayuni.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha