Abu Ubaida, Msemaji wa Brigedi za al-Qassam, amebainisha hayo katika hotuba iliyorekodiwa kwa video na kurushwa hewani Alkhamisi usiku akisisitiza kwamba kile ambacho utawala ghasibu wa Kizayuni umeshindwa kukipata kupitia "silaha na vita" hautaweza kamwe kukipata kwa "vitisho na hila".
Msemaji wa Al-Qassam ametoa tamko hilo siku moja tu baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kwamba Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza na wapiganaji wa Hamas watauawa ikiwa hawatawaachilia mara moja mateka waliosalia wa Israel wanaoshikiliwa katika eneo hilo la Palestina lililowekewa mzingiro.
Abu Ubaida amefafanua kuwa, licha ya ukiukaji wa makubaliano na usaliti unaofanywa na adui Mzayuni, Hamas imeendelea kuheshimu na kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo ya kubadilishana mateka na kuithibitishia hilo dunia na wapatanishi.
Msemaji wa Al-Qassam ameongezea kwa kusema: "tumeamua - na tungali tunataka - kushikamana na makubaliano haya ili kuzuia umwagaji wa damu ya watu wetu, kuondoa visingizio vyovyote, na kuheshimu ahadi tulizotoa kwa wapatanishi".
Katika sehemu nyingine ya tamko hilo la tawi la kijeshi la Hamas, Abu Ubaida ametoa indhari kwa kusema: "Umma wa Kiislamu hautapata amani au utulivu, wala hautakuwa na nafasi ya kuheshimika miongoni mwa mataifa, hadi ardhi hii takatifu (Palestina) itakaposafishwa kwa (kuondolewa) Wazayuni maghasibu".
Vile vile amesisitiza kuwa, njia fupi zaidi ya kupatikana uthabiti na amani katika eneo ni "kuudhibiti utawala wa Kizayuni" na kuulazimisha utekeleze ahadi zake ulizosaini kuwa utazitimiza.
Msemaji wa Al-Qassam ametahadharisha kwa kusema: "kitisho anachotoa adui cha kurejea vitani kitatusukuma tu kurudi kwenye medani ya vita ili kumaliza mabaki ya itibari yake," na akasisitiza kwamba vitisho unavyotoa utawala wa Kizayuni vinadhihirisha udhaifu wake tu na fedheha uliyopata.
Aidha ametoa indhari kwamba kushadidi uchokozi wowote mpya utakaoanzishwa na jeshi la Kizayuni kunaweza kusababisha mauaji kwa baadhi ya mateka waliosalia wa adui Mzayuni.../
342/
Your Comment