Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Ismail Baqae sanjari na kuashiria juhudi za Iran za kutaka kufanya kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiislamu amesema kuwa, mpango wa kuwahamisha kwa nguvu watu wa Gaza kutoka Palestina inayokaliwa kwa mabavu, ni muendelezo wa mauaji ya kimbari kwa kutumia njia nyingine, yaani kwa kutumia vyombo vya kisiasa.
Akizungumza katika mahojiano ya televisheni kuhusu mahitaji, maelezo na ajenda za mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu, Baqae amesema kuwa, madhumuni ya ombi la kufanyika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ni kutaka kuitanabahisha OIC, ikiwa ndiyo jumuiya muhimu zaidi katika Ulimwengu wa Kiislamu, katika suala ambalo linaitia wasiwasi mkubwa jamii na nchi za Kiislamu, na suala lenyewe ni hatari ya kuendelea mauaji ya halaiki ya Wapalestina, haswa watu wa Gaza.
Baqae ameongeza kwa kusema, "Pia, ajenda nyingine itakuwa ni kuchunguza matukio hatarishi yanayoshuhudiwa katika Ukingo wa Magharibi. Falsafa muhimu zaidi ya kuwepo kwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu ni kadhia ya Palestina, yaani, tangu mwanzo wa kuanzishwa kwa OIC, ilikuwa ni kushughulikia kadhia ya watu wa Palestina, ambayo ilikuwa ni juhudi za kupata haki, mamlaka na uhuru wa kujitawala."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, mantiki inahukumu kwamba, shirika la OIC linapaswa kufanya mkutano kwa kuzingatia hali ya hivi sasa, ambapo wananchi wa Palestina wanakabiliwa na mgogoro usio na kifani. Ameongeza kuwa, mgogoro ambao ulikabiliwa vyema na mhimili wa Muqawama katika kipindi cha miezi 17 ya "mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni", hivi sasa unafanyika kwa njia tofauti, kwa kutumia zana za kisiasa.
342/
Your Comment