12 Machi 2025 - 18:27
Source: Parstoday
Yemen yaanza tena kushambulia meli za Israel baada ya kukataa kufungua vivuko vya Ghaza

Yemen imetangaza kuanza tena operesheni za kijeshi za kushambulia meli za Israel katika maeneo muhimu ya baharini karibu na fukwe zake kufuatia kumalizika muda wa mwisho ilioupa utawala wa Kizayuni wa kufungua tena vivuko vya Ukanda wa Ghaza na kuruhusu misaada kuwafikia Wapalestina iliowasababishia hasara kubwa kutokana na mashamblizi yake ya kikatili ya zaidi ya miezi 15.

Mapema leo Jumatano, wanajeshi wa Yemen wametangaza kuwa mashambulizi hayo yataanza tena kwa mujibu wa amri iliyotolewa na Kiongozi wa Harakati ya Muqawama ya Ansarullah, Sayyid Abdul Malik al-Houthi.

Kwa upande wake, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imefurahishwa na hatua ya Harakati ya Wananchi wa Yemen ya Ansarullah ya kuipa Israel muda wa siku nne ihakikishe imeruhusu misaada inaingia Ghaza, vinginevyo itaanza tena operesheni za jeshi la majini dhidi ya meli zenye uhusiano na Israel katika Bahari Nyekundu.

Israel imetia ulimi puani kupitia kuzuia misaada kuingia kwenye Ukanda wa Ghaza, tofauti kabisa na makubaliano ya kusimamisha vita iliyofikia na HAMAS. Kitendo hicho cha utawala wa Kizayuni kimekusudia kuongeza mashinikizo kwa Wapalestina huko Ghaza, ambao tayari wanaendelea kuteseka kutokana na miezi 15 ya mashambulizi na mauaji ya umati yaliyofanywa na Israel dhidi yao.

Amri ya jeshi la Yemen inasema: Kuanzia sasa, meli zote za Israel haziruhusiwi kuvuka maeneo yaliyoainishwa na jeshi la Yemen kufanyia kazi zake ikiwa ni pamoja na Bahari ya Sham (Bahari Nyekundu), Bahari ya Arabia, Lango-Bahari la Bab al-Mandab na Ghuba ya Aden.

Vikosi hivyo vimeonya kwamba meli zozote za Israel zitakazojaribu kupuuuza marufuku hiyo zitapigwa kwa silaha za jeshi la Yemen.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha