Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Leo hii - Ijumaa - Tarehe 25 Julai - 2025, sawa na Tarehe 29 Muharram, 1447 Hijria, Dua ya Nudba imesomwa katika Madrasa ya Mabinti (Madrasat al-Akhawat) ya Hazrat Sayyidat Zainab (SA) iliyopo Kigamboni - Jijini Dar-es-salaam.
Majlisi hii ya kiroho ilihusu usomaji wa Dua ya Nudba, ambayo kwa hakika ni dua maarufu ya matarajio na matumaini ya kudhihiri kwa Imam wa Zama (a.t.f.s), ambayo husomwa kila Siku ya Ijumaa katika ukumbi wa Madrasa hii ya mabinti wa Kiislamu.
Dua hiyo ilisomwa kwa adabu na utulivu na unyenyekevu wa hali ya juu huku Mabinti hawa wa Kiislamu wakiwa wamekusanyika kwa pamoja kwa lengo la kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kuonyesha hamu ya dhati ya kudhihiri kwa Imam Mahdi (a.t.f.s).
Katika dua hiyo, kwa namna ya Usomwaji wake, nyoyo za Wanafunzi hawa wa Kiislamu ziliungana kwa vilio vya upendo, huzuni na matumaini.
Walimu waliandaa mazingira ya utulivu wa kiroho, na dua ilisomwa kwa hisia, ikifuatiwa na mawaidha mafupi kuhusu maana ya kusubiri (kungojea) na nafasi ya Imam Mahdi (a.t.f.s) katika maisha ya kila Muislamu.
Taarifa ya Mahudhurio:
Idadi ya wahudhuriaji: Takriban Wanafunzi 70 wa Kike.
Kundi lililolengwa katika Malezi ya Usomaji Dua na Utamaduni huu wa kuwasiliana na Mwenyezi Mungu kupitia Dua ni: Wanafunzi wa kike, Walimu na wahudumu wa Madrasa husika.
Nukuu Muhimu:
"Dua ya Nudba ni kilio cha roho inayotamani haki irejee. Ni kilio cha wale waliomsubiri Imam wao wa Zama kwa subira na msimamo."
Ni maneno mazuri yaliyosikika katika mawaidha yaliyowasilishwa na kufafanuliwa baada ya kumaliza kusoma Dua hii ya Nudba.
Mapendekezo ya Baadaye kwa Kila Muislamu ni:
1_ Kuendeleza Usomaji wa Dua hii kila Ijumaa ya Mwisho wa Mwezi.
2_ Kutoa maelezo ya maana ya kila sehemu ya dua kwa Wanafunzi.
3_ Kuwashirikisha wazazi na jamii kwa ujumla (panapo uwezekano wa hilo).
Tunamwambia Imam wetu Mahdi (a.t.f.s), kwamba: Tuko tayari kwa moyo, kwa dua, na kwa matendo!.
Imetayarishwa na:
Kitengo cha Habari na Ripoti – Madrasa ya Mabinti ya Hazrat Zainab (SA) - Kigamboni, Dar-es-salaam.
Tarehe: 25 Julai 2025
Your Comment