Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa mashambulizi yaliyofanywa na Israel kwa kushirikiana na Marekani yamekuwa sababu ya kuleta mshikamano wa kitaifa usio na mfano katika historia ya hivi karibuni ya nchi hiyo.
"Mashambulizi haya hayakuwa tu jaribio la kutudhuru, bali yamefichua sura halisi ya adui na kusababisha mwamko mkubwa wa umoja miongoni mwa wananchi wetu," alisema Rais. "Hata wale waliokuwa wakitukosoa au kutupinga waziwazi sera zetu, leo hii wamesimama pamoja nasi kwa moyo mmoja."
Rais alisisitiza kuwa taifa la Iran limejifunza kupitia historia yake kuwa katika nyakati za shinikizo na hujuma za kigeni, mshikamano wa kitaifa ndio silaha kubwa zaidi ya kujilinda.
"Leo tunashuhudia kwa macho yetu kuwa kila Muirani - awe ni mfuasi wa Serikali au mpinzani wake - amekuwa sauti moja katika kutetea hadhi, uhuru, na mamlaka ya nchi yetu. Hii ni neema iliyojificha katika madhila, na tunaamini kwa yakini kuwa mshikamano huu utakuwa msingi wa ushindi wetu wa baadaye."
Taarifa hiyo imekuja katika kipindi cha taharuki kubwa kufuatia mashambulizi ya kijeshi ambayo yamesababisha hofu ya mzozo mkubwa zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Your Comment