Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Ustadhi Abdallah Amani ametoa nasaha zenye hekima kwa wanandoa, akionya juu ya kile alichokitaja kuwa kifungo kibaya zaidi katika maisha ya ndoa.
Katika maelezo yake, Ustadhi Amani amesema: “Kifungo kibaya katika maisha ya ndoa ni kurudia mambo yale yale, kwa maana kila siku kuwa kama jana. Wakati ambapo maisha yanapokuwa ya kawaida kupita kiasi, na yasiwe na mabadiliko yoyote, hutokea yafuatayo: Mwanaume humchoka Mwanamke na Mwanamke humchoka Mwanaume, na mwisho wa siku wote wawili huchokana.”
Amebainisha kuwa hali hiyo huanza taratibu, lakini huathiri sana mshikamano wa kifamilia na mapenzi ya wanandoa, endapo haitatambuliwa mapema.
Aidha, Ustadhi Abdallah Amani amesisitiza kuwa: “Maisha ya ndoa yanahitaji uhai, ubunifu, mabadiliko madogo, na msisimko wa pamoja ili yasigeuke kuwa kifungo cha uchovu.”
Kwa mujibu wake, juhudi za pande zote mbili katika kuhuisha mawasiliano, kuleta ubunifu katika maisha ya kila siku, na kuthaminiana, ndizo nguzo muhimu za kudumisha ndoa yenye utulivu, furaha na baraka.
Nasaha hizi zinakuja kama wito kwa wanandoa kutafakari kwa kina mwenendo wa maisha yao ya ndoa, na kuchukua hatua za makusudi ili kulinda Uhai wa Ndoa yao tukufu dhidi ya uchovu na kusinyaa kwa mapenzi na Mahusiano ya Ndoa.

Your Comment