Duru hiyo imenukuliwa na televisheni ya SkyNews ya Kiarabu ikieleza kwamba: "Hamas haijapendekeza wazo la kujiondoa katika siasa na kuweka chini silaha mkabala wa kutekelezwa usitishaji vita wa muda mrefu utakaodumu kwa muda wa kati ya miaka mitano hadi kumi."
Chanzo hicho kimeongeza kuwa "wazo la Hamas kujiondoa katika siasa na kuweka chini silaha mkabala wa kufikia mapatano ya kusitisha vita huko Ghaza kwa muda mrefu lilipendekezwa na ujumbe wa Marekani lakini lilikataliwa na harakati hiyo."
Chanzo hicho kimeendelea kueleza: "Hamas ilionyesha ulainifu na kukubali kuwaachilia mateka kumi mkabala wa kusitishwa mapigano kwa miezi miwili, lakini Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alikataa pendekezo hilo, na kupelekea kusitishwa utekelezaji wake."
Duru hiyo ya Palestina imebainisha kuwa, Hamas ilipendekeza pia kumwachilia raia wa Marekani Aidan Alexander kama harakati ya kuonyesha nia njema, bila ya kufanyika hafla rasmi ya makabidhiano, ili kufungua mazungumzo na Washington.
Mapema, Adam Boehler, mjumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump katika masuala ya mateka, alifichua baadhi ya yaliyozungumzwa katika mikutano aliyofanya na Hamas ili kufikia mwafaka kuhusu Ghaza, akielezea mazungumzo hayo kuwa "ya kusaidia sana."
Katika mahojiano, Boehler alidai kwamba, Hamas imejitolea kuwaachilia mateka wote mkabala wa kusitishwa mapigano utakaodumu kwa muda wa kati ya miaka mitano hadi kumi.
Aidha, Boehler alisema, mateka wa pande zote mbili wataachiliwa, usitishaji vita wa muda mrefu utafikiwa, na eti Hamas itapokonywa silaha, na vilevile kundi hilo la ukombozi wa Palestina litajitenga na masuala ya kiutawala ya Ghaza.../
342/
Your Comment