Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imemuita Irfan Siddiq, balozi wa Uingereza, ili kuwasilisha malalamiko rasmi kuhusiana na matamshi yake kuhusu ushiriki wa Hashd al-Shaabi ndani ya mfumo wa usalama wa Iraq.
Muhammad Hussein Bahr al-Uloom, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq anayeshughulikia masuala ya pande mbili, alieleza wasiwasi mkubwa wa serikali ya Iraq kuhusu kauli hizo na kusisitiza kwamba maneno hayo yanakinzana na Mkataba wa Vienna kuhusu mahusiano ya kidiplomasia.
Alisisitiza umuhimu wa wawakilishi wa kidiplomasia kuheshimu sheria za nchi mwenyeji na kuepuka kuingilia masuala ya ndani. Msimamo huo umetolewa rasmi kupitia taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq.
Serikali ya Iraq pia imemtaka balozi wa Uingereza kuepuka kutoa kauli kama hizo au kufanya vitendo vinavyofanana katika siku zijazo, na badala yake ajitahidi kuimarisha uhusiano wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili.
Mwisho wa taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imesisitiza umuhimu wa kuheshimiana na kutoingilia masuala ya ndani, sambamba na kuendeleza mawasiliano ya kidiplomasia yenye tija.
Inapaswa kutajwa kuwa mnamo tarehe 8 Agosti mwaka huu, Irfan Siddiq, balozi wa Uingereza nchini Iraq, alisema kwamba nchi yake haina pingamizi kuhusu uwepo wa Hashd al-Shaabi ndani ya mfumo wa usalama wa Iraq, lakini ina wasiwasi juu ya baadhi ya makundi yanayofanya shughuli nje ya mamlaka ya serikali, akiyataja kama tishio kwa usalama na uthabiti wa Iraq.
Your Comment