Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- – Nasif Jasim Al-Khattabi, Gavana wa Karbala, alisema kuwa mpango huo wa kigaidi uliolenga mahujaji wa Arubaini wa Imam Hussein (a.s) umefanikiwa kuzuiwa.
Kulingana na Shirika Rasmi la Habari la Iraq (INA), Al-Khattabi katika mkutano na waandishi wa habari alibainisha kuwa kikosi cha kijasusi cha "Saqur" katika mkoa wa Karbala, kwa usimamizi wa moja kwa moja wa Mahakama ya Uchunguzi ya Karbala, kilifanya operesheni ya kijasusi kwa usiri na umakini wa hali ya juu.
Akaongeza kuwa, matokeo ya operesheni hiyo yalikuwa kukamatwa kwa magaidi 22 waliokuwa wakipanga kufanya vitendo vya jinai, vikiwemo kuweka mabomu kando ya barabara zinazotumiwa na mahujaji, kushambulia vikosi vya usalama na mahema ya maombolezo ya Husseini, pamoja na kujaribu kuweka sumu katika maeneo ya mikusanyiko ya mahujaji, hasa katika barabara ya kusini ya mkoa huo.
Gavana wa Karbala aliendelea kusema kuwa miongoni mwa mipango iliyozuiwa kulikuwa na jaribio la kulenga moja ya Husayniyya katika njia ya kutoka Karbala hadi Najaf, lakini njama hiyo ilishindikana kutokana na ushirikiano wa taasisi za mahakama na usalama.
Alisisitiza kuwa watuhumiwa walikuwa na nyaraka na ushahidi unaothibitisha nia zao za kigaidi, na wamekiri mahakamani kuwa ni wanachama wa kundi la kigaidi la ISIS.
Akaongeza kuwa baadhi ya watuhumiwa walikuwa na mawasiliano na pande za kigeni, akiwemo mtu mmoja aliyekuwa akiwasiliana moja kwa moja na utawala wa Kizayuni na wale wanaounga mkono ugaidi.
Al-Khattabi alihitimisha kwa kusisitiza kuwa juhudi za kiusalama za kuwalinda mahujaji na kuhakikisha mazingira salama katika matukio yajayo ya kidini zinaendelea.
Your Comment