9 Agosti 2025 - 18:15
Kiongozi Mwandamizi wa Hezbollah Lebanon: "Kufa ni bora kuliko kukabidhi silaha za upinzani"

Uamuzi wa Serikali unaweza kugeuza tatizo kutoka mapambano kati ya Lebanon na Israel na kuwa mzozo wa ndani.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kiongozi wa Kambi ya “Uaminifu kwa Upinzani / Muqawama” katika Bunge la Lebanon, akijibu uamuzi wa Serikali ya nchi hiyo wa kulipokonya silaha Jeshi la Upinzani (Hezbollah), amesema kuwa kufa ni bora kuliko kukabidhi silaha. Na ameonya juu ya athari zisizotabirika za uamuzi wa kulipokonya silaha Jeshi la Upinzani (Muqawama wa Hezbollah) katika hali ya ndani ya Lebanon.

Akizungumza na kituo cha televisheni cha Al-Manar, Raad alisema kuwa uamuzi wa serikali wa kupokonya silaha Upinzani ni uamuzi wa haraka uliowekwa kwa shinikizo la Marekani. Amesema uamuzi huu wa kiserikali umepoteza uhalali wa kitaifa, ni hatari, unadhoofisha mamlaka ya Lebanon, na unampa adui nafasi ya kuichezea amani ya ndani.

Amesisitiza: “Kukabidhi silaha ni sawa na kujiua, na sisi hatuna nia ya kujiua.” Amesema serikali inaweza kutumia uwezo wake kuonyesha mamlaka yake, lakini haina uwezo wa kukabiliana na majeshi ya uvamizi.

Raad alirudia msimamo wa Hezbollah kwamba silaha zinaweza kuwa mikononi mwa Serikali pekee endapo Serikali itakuwa na uwezo wa kulazimisha wavamizi kuondoka na kulinda Taifa.

Ameonya kuwa uamuzi huu unaweza kugeuza tatizo kutoka mapambano kati ya Lebanon na Israel na kuwa mzozo wa ndani.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa Hezbollah inashikamana na amani, lakini uamuzi huu ni hatari: “Tunawezaje kuwa na uhakika kuhusu matokeo yake?” alihoji.

Kuhusu uwezekano wa mawaziri wa Hezbollah kujiondoa Serikalini, Raad amesema: Serikali ina mambo chanya katika baadhi ya nyanja, hasa katika baadhi ya wizara, lakini kubaki au kuondoka Serikalini ni uamuzi wa Hezbollah.

Aidha, amesisitiza kuwa fedha yoyote itakayotolewa baada ya kukabidhi silaha kwa ajili ya ujenzi upya, ni fedha haramu na isiyokubalika. “Msaada kutoka kwa wale waliokuwa washirika katika kumwaga damu yetu ni wa kukataliwa,” amesema.

Mwisho, Kiongozi wa Kambi ya “Uaminifu kwa Upinzani” ametoa kauli yake binafsi: “Kufa ni bora kuliko kukabidhi silaha.”

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha