8 Machi 2025 - 17:32
Source: Parstoday
Araghchi: Kuundwa nchi moja ya kidemokrasia ndiyo suluhu ya kadhia ya Palestina

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesisitiza tena msimamo wa Tehran wa kupinga eti 'suluhisho la mataifa mawili' kuwa njia ya kupata haki za Wapalestina na kusisitiza kwamba, uungaji mkono usioyumba wa Iran kwa kadhia ya Palestina bado upo thabiti.

Akizungumza jana Ijumaa katika kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) huko Jeddah, Saudi Arabia, kilichoitishwa kuchunguza uvamizi na jinai za Israel dhidi ya watu wa Palestina, Araghchi amesisitiza misimamo thabiti ya Iran kuhusu Palestina na kubainisha kuwa uungaji mkono wa Tehran kwa Wapalestina "haupingiki."

"Uungaji mkono usiobadilika wa serikali na wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kadhia ya Palestina ni jambo lisilopingika na dhamira yetu thabiti haitanyauka kwa hali yoyote ile," ameongeza. Kadhalika amepuuzilia mbali "suluhisho la serikali mbili," akieleza bayana kuwa kuundwa "nchi moja ya kidemokrasia" ndiyo suluhisho pekee linalowezekana kwa kadhia ya Palestina.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema kutimuliwa Wazayuni maghasibu na kurejea Wapalestina katika ardhi za mababu zao ndilo suluhisho pekee la mgogoro wa Palestina-Israel.

Araghchi: Kuundwa nchi moja ya kidemokrasia ndiyo suluhu ya kadhia ya Palestina

Ameeleza kuwa, "Kwa kuheshimu maoni ya baadhi ya nchi ndugu kuhusu 'suluhisho la serikali mbili', Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inashikilia mtazamo wake kwamba suluhisho hili halitapelekea kupatikana kwa haki za watu wa Palestina."

Aidha Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani "uungaji mkono usioyumba na usio na masharti" wa Marekani na washirika wake wa Magharibi kwa Israel katika vita vyake dhidi ya Gaza. Akitoa mfano wa uungaji mkono wa kijeshi, kifedha na kidiplomasia wa Washington dhidi ya Tel Aviv, Araghchi amesisitiza kuwa, matukio ya Gaza yanadhihirisha wazi ushiriki wa Marekani katika jinai zinazofanywa na Israel.

Your Comment

You are replying to: .
captcha