Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ya Umma nchini humo imesema katika taarifa kuwa: Moto huo ulizuka na kuenea kwa kasi hadi kwenye dari na paa la klabu hiyo ya usiku. Taarifa hiyo imeeleza kuwa, "Tungali tunatathmini idadi ya wahanga na majeruhi wa mkasa huo wa moto huo."
Shirika la Serikali la Kukabiliana na Majanga MIA likirejelea taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani limesema kuwa, takriban watu 50 wameuawa kwenye janga hilo.
Shirika hilo limeripoti kuwa, moto huo ulizuka katika Klabu ya Pulse, ukumbi wa starehe uliopo katika mji huo mdogo wenye wakazi takriban 30,000, wakati wa tamasha la kundi la DNK, ambalo ni la wanamuzi maarufu wa kufokafoka nchini humo.
Aghalabu ya waliohudhuria tamasha hilo lililoanza usiku wa manane mnamo Machi 16, ni tabaka la vijana. Tovuti ya habari za mtandaoni ya SDK imeripoti kuwa, moto huo ulianza saa tisa usiku wa kuamkia leo. Ikinukuu vyanzo vya uokoaji, tovuti hiyo imesema zaidi ya watu 100 wamejeruhiwa kwenye moto huo.
Habari zaidi zinasema kuwa, waliojeruhiwa wamepelekwa katika hospitali ya eneo la Kocani au Stip, umbali wa kilomita 30 kusini mwa mji.
342/
Your Comment