17 Machi 2025 - 18:12
Source: Parstoday
Sisitizo la Iran la kukabiliana na siasa za mabavu za Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi alisema Jumapili, Machi 16, katika kujibu matamshi ya kibabe na ya uingiliaji ya viongozi wa Marekani dhidi ya Iran, kwamba serikali ya Washington haina haki ya kuilazimisha Iran itekeleze siasa za kigeni zinazoendana na maslahi ya Washington.

Akiwahutubu viongozi wa Marekani, Araghchi amesema zama za kuilazimisha Iran itekeleze siasa fulani ziliisha mwaka 1979. Amewaambia viongoi hao kwamba: "Acheni kuunga mkono mauaji ya kimbari na ugaidi wa Israel. Acheni kuua watu wa Yemen." Rais Donald Trump wa Marekani aliamuru mashambulizi mapya dhidi ya Yemen Jumamosi usiku, Machi 15, hivyo nchi hiyo na Uingereza zimeanzisha duru mpya ya mashambulizi dhidi ya Yemen. Nukta ya kuzingatiwa ni kwamba maafisa wakuu wa usalama na kijeshi wa serikali ya Trump wamezitishia Iran na Yemen baada ya mashambulizi ya kinyama katika maeneo ya raia, ambayo yamepelekea watu wasio na hatia kupoteza maisha. Kuhusiana na hili, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani Mike Waltz amesema: "Urithi tuliorithi kutoka kwa serikali ya zamani ni mbaya sana. Chaguzi zote dhidi ya Iran ziko mezani na Iran inapaswa kuacha kuwaunga mkono Mahouthi (Ansarullah ya Yemen)." Pete Hegseth, Waziri wa Ulinzi wa Marekani pia amedai: "Mashambulizi yataendelea hadi hatua za kijeshi za Wahouthi zisimame...Iran imekuwa ikiwasaidia Wahouthi kwa muda mrefu na ni bora kuacha kufanya hivyo."

Tuhuma mpya za maafisa wa utawala wa Trump kuhusu uungaji mkono wa Iran kwa Ansarullah ya Yemen, na vilevile tishio kwamba chaguzi zote dhidi ya Iran ziko mezani, kwa hakika ni muendelezo wa siasa ambazo Marekani imekuwa ikizitekeleza dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa miongo kadhaa. Hasa sentensi ya kukaririwa ya eti "chaguzi zote dhidi ya Iran ziko mezani", ni sentensi ambayo marais wote wa Marekani kuanzia George Bush na Barack Obama hadi Joe Biden na Donald Trump wamekuwa wakiitumia mara kwa mara. Lengo lao siku zote limekuwa jambo moja, ambalo ni kuitisha Iran kupitia siasa za mabavu na misimamo ya kuamrisha. Hata baada ya barua ya hivi karibuni ya Trump kwa Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Marekani haijaacha kutumia lugha hiyo isiyo ya kimantiki.

Sisitizo la Iran la kukabiliana na siasa za mabavu za Marekani

Hata hivyo Iran haijawahi kusalimu amri mbele ya vitisho vya Marekani na jibu la Iran kuhusiana na hilo limeelezwa wazi na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Siku moja baada ya kutangazwa habari ya kutumwa barua ya Trump, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema: “Ukweli kwamba baadhi ya serikali za kibabe zinasisitiza juu ya mazungumzo, mazungumzo yao si ya kutatua matatizo bali ni kwa ajili ya kutawala wengine. Mazungumzo yafanyike ili kuulazimisha upande wa pili ukubali wanachokitaka kupitia mazungumo." Amesisitiza: "Mazungumzo yanayofuatiliwa na Marekani hayataishia kwenye mpango wa nyuklia wa Iran tu. Serikali hizi hazina nia ya kufanya mazungumzo ya kutatua masuala na wanataka kutawala na kulazimisha." Ayatullah Khamenei ameendelea kusema: “Wanapendekeza matarajio mapya ambayo kwa hakika hayatatimizwa na Iran; Usifanye hiki na kile kuhusu zana za ulinzi wa nchi na uwezo wa kimataifa wa nchi, usikutane na mtu fulani, msiimarishe masafa ya makombora yenu kufikia kiwango fulani."

Juhudi za marais wa Marekani hususan Donald Trump zimekuwa ni kuweka vikwazo vikali na vikubwa zaidi dhidi ya Iran ili kudhibiti na hatimaye kuilazimisha ikubali matakwa haramu na yasiyo na mantiki ya Marekani ikiwemo sekta ya teknolojia ya nyuklia, siasa za kieneo na uwezo wake wa makombora. Mtazamo wa utawala wa Biden ulikuwa kwa namna ambayo ulikuwa mwendelezo wa mtazamo wa kimabavu wa utawala wa Trump kuhusiana na Iran, mtazamo ambao bila shaka umethibitishwa kutofanya kazi. Kufuatia kuingia tena Trump White House, siasa zile zile za zamani, yaani za kutoa mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Tehran, zimeanza kutekelezwa tena kwa kiwango kikubwa zaidi, ambapo kipengele kipya cha vitisho vya kijeshi dhidi yake, pia kimeongezwa. Siasa hizo bila shaka zilishindwa wazi katika muhula wa kwanza wa utawala wake.

Sasa maafisa wakuu wa usalama na kijeshi wa utawala wa Trump kwa kutumia lugha ile ile ya zamani, wamerudia vitisho dhidi ya Iran na Ansarullah ya Yemen ambazo ni sehemu ya mhimili wa muqawama. Hata hivyo, majibu ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa vitisho vipya vya maafisa wakuu wa Marekani yamesisitiza kuwa, serikali ya Marekani haina haki ya kuitwisha Iran sera zake za kigeni. Amesema zama za kulazimishwa siasa hizo zilimalizika wakati wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, jambo linalothibitisha kwamba Iran kamwe haitasalimu amri mbele ya vitisho vya Marekani, na kuwa itaendelea kufuata njia ya mapambano na muqawama kama ilivyofanya katika miaka 45 iliyopita ambapo imevumilia kila aina ya vikwazo vikubwa, njama na vitendo vya uadui vya nchi hiyo ya Magharibi.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha