17 Machi 2025 - 18:22
Source: Parstoday
UNICEF: Asilimia 90 ya wakazi wa Ghaza wanashindwa kupata maji safi ya kunywa

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetahadharisha kuwa uhaba mkubwa wa maji katika Ukanda wa Ghaza umefikia hatua mbaya na ya maafa, kwa ababu karibu asilimia 90 ya wakazi wa eneo hilo wanashindwa kupata maji safi ya kunywa.

Rosalia Bollen, mwakilishi wa UNICEF katika Ukanda wa Ghaza, ametangaza kwamba mnamo Novemba 2024, watu wapatao 600,000 waliweza kupata tena maji ya kunywa, lakini uwezo huo wa kupata maji umekatishwa tena.

"Tunakadiria kuwa watu milioni 1.8, zaidi ya nusu yao wakiwa ni watoto, wanahitaji maji haraka sana, pamoja na huduma za afya na misaada ya tiba," ameeleza Bollen. Hali hiyo mbaya ya uhaba wa maji imeshtadi baada ya kukatwa umeme katika Ukanda wa Ghaza na kusababisha mitambo ya kuondoa chumvi kwenye maji kusita kufanya kazi.

Afisa huyo wa UNICEF ameongezea kwa kusema: "ni mtu mmoja tu kati ya 10 katika Ukanda wa Ghaza anayepata maji safi ya kunywa".

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limetangaza kuwa mnamo tarehe 2 Machi, utawala ghasibu wa Israel ulisimamisha uingizaji misaada ya kibinadamu ndani ya Ghaza ikiwa ni pamoja na mafuta; na tangu wakati huo hadi sasa hakuna shehena yoyote ya misaada ya kibinadamu au ya kibiashara iliyoingizwa katika eneo hilo.

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Muhand Hadi naye pia ametahadharisha kuwa, uingizaji misaada yenye umuhimu mkubwa sana huko Ghaza inapasa uanze mara moja.

Hadi amesisitiza kuwa: ucheleweshaji wowote zaidi utaofanywa, utavuruga mafanikio yote yaliyopatikana wakati wa usitishaji vita.

Katika wiki za karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel umekabiliwa na ongezeko la mashinikizo ya kimataifa ya kuutaka upunguze mbinyo wa hali mbaya ya kibinadamu inayoshuhudiwa huko Ghaza, lakini kwa uamuzi wake mpya uliochukua, umezidisha uwezekano wa kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu katika eneo hilo. Wakati huo huo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yametahadharisha juu ya matokeo mabaya ya hatua hiyo ambayo yameitaja kuwa ni mfano wa wazi wa utoaji adhabu ya pamoja dhidi ya raia kwa waliomo na wasiokuwemo.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha