Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (AS) – Abna – Katika upande wa Mume, kimsingi hakuna shaka wala mkanganyiko wowote(yaani, kisheria Mume anaruhusiwa kufunga saumu yoyote bila kuhitajia idhini ya Mkewe), na katika upande wa Mwanamke, baadhi ya Mafaqihi wamesisitiza kuwa Mwanamke anaruhusiwa kutekeleza Funga / Saumu yake ya Faradhi (Wajibu) bila ya kuhitajia idhini ya Mumewe, na wala haijuzu kwa Mume kumzuia (kufunga).
Hata hivyo, ikiwa Funga (Saumu) ya Faradhi ina muda mpana zaidi na haiishii au haikomei katika muda au siku maalum, mfano Funga (Saumu) ya Qadhaa (Kulipa), ambayo imebakia zaidi ya idadi ya siku kadhaa za Qadhaa kutoka miaka ya nyuma au hadi Ramadhani ijayo (bado kuna siku kadhaa zimebakia kabla ya Ramadhan), ikiwa Mwanamke anataka kuifanya (kuifunga Saumu hiyo) kabla ya muda wake wa kuifunga kukaribia kuisha, je Mume wake anaweza kumzuia?.
Al-Allama al-Hilli alitilia ishkali na shaka katika hilo. Kabla yake, Sheikh Mufid alisema kuwa ni Makruh (jambo lenye kuchukiza) kwa Mwanamke kufunga pasina kuwa na idhini ya Mumewe. Hata hivyo anasema pia kuwa Mume haruhusiwi kumzuia Mkewe kufunga saumu ya Qadhaa isipokuwa ikiwa bado kuna muda wa kutosha (kiasi kwamba Mke anaweza kufunga kesho au hata baadae).
Hata hivyo, Mirza Qomi aliichukulia hukumu hiyo (iliyoelezwa hapo juu) kuwa ni makhsusi kwa ajili ya funga (Saumu) ya Mustahabu, ama ikiwa ni Saumu (Funga) ya Wajibu, hata kama bado Saumu hiyo ina (muda mpana, unaoruhusu kuhairisha au kuchelewesha kufunga), hahitajii Mke kuomba idhini ya Mumewe (pindi atakapotaka kuifunga). Inaweza kusemwa kwamba Mafaqihi wengi waliosema kuwa Mwanamke hawezi kufunga wakati wa Saumu ya “Mustahabu” bila ya “Ruhusa / Idhini” ya Mume wake au kwa “Kukatazwa” na Mume wake, waliichukulia hukumu hiyo kuwa ni makhsusi kwa hiyo Saumu tu (yaani: Saumu au Funga ya Mustahabu), na kuiondoa Funga ya Wajibu katika mjadala huu kabisa.
Vyovyote iwavyo, kilichojipatia umaarufu mkubwa miongoni mwa Mafaqihi na hata kufikia kudai Ijma'u (itifaki katika hilo) ni kwamba Mwanamke hawezi kufunga funga (saumu) iliyopendekezwa (Saumu ya Mustahabu) bila ya idhini ya Mumewe. Hata hivyo, wengine wanasema (anaweza kufunga bila ya idhini ya Mume wake saumu ya mustahabu, lakini) ni Makruhu (ni jambo lenye kuchukiza). "Sayyid Murtadha", "Ibn Hamza", na "Sallar Deylami" wanatoka katika kundi hili.
“Sayyid bin Zuhrah” aliona kuwa ni Mustahabu (jambo linalopendekezwa) kwa Mwanamke kuomba ruhusa (idhini kutoka kwa Mumewe) na hata akadai Ijma'u (itifaki) juu ya maoni haya. Wengine wamesema kuwa kuna tofauti kati ya uwepo wa katazo la Mume na kutokuwepo kwake. Katika sura ya kwanza, ikiwa Mke atafunga (wakati lipo katazo la mumewe), basi saumu yake sio sahihi (ni batili). Shahidi wa Kwanza ametoa maoni kama hayo (Muhammad bin Jamal al-Din Makki A'mili (734-786 AH) anajulikana kama Shahidi wa Kwanza miongoni mwa Mafaqihi wa Kishia katika karne ya 8). Sahib Riyad (Sayyid Ali bin Muhammad Ali (Muhammad) Tabatabai Haeri (1161-1231 AH), anayejulikana kama Sahib Riyadh, ni mmoja wa Mafaqihi na Wana Usul wa Kishia katika karne za 12 na 13 za kalenda ya Hijria) pia ameibua (au ameshikamana na) uwezekano wa hilo na akazingatia uhakika huo kuwa hilo ni jambo liko wazi kwamba Saumu yake inakuwa batili endapo kutakuwepo katazo la Mume wake, vinginevyo (bila kuwepo katazo lolote la Mumewe), itakuwa ni Makruhu (ni jambo lenye kuchukiza) tu, na itakuwa ni (kwenda) kinyume na Ihtiyat (tahadhari).
Kuna (tafsiri au) maelezo mengine katika suala hili, kati ya Kuvuruga (kuleta zahma) na Kutovuruga (kutokuleta zahma kwenye) Haki ya Mume. Mafaqihi wa zama hizi, wanaomfuata Faqihi wa Yazdi, Mwandishi wa `"Ur'wat al-Wuthqa", kwa ujumla wao wameshikilia rai hiyo hiyo, ingawa wameona kuwa kwa ajili ya hadhari (Ihtiyat) Mwanamke asifunge bila ya ruhusa / idhini ya Mume wake, na ikiwa Mume amemkataza kufanya hivyo (kufunga), hata ikiwa (funga hiyo) haiingiliani (haivurugi, haileti zahma, haizuii) na haki zake, Mafaqihi hao wamesisitiza kwamba tahadhari (Ihtiyat) isiachwe.
Kumbuka: Mume hawezi kuzuia funga (saumu) ya faradhi (wajibu) kwa njia yoyote ile. Ifahamike kuwa hakuna mtu ana haki ya kumzuia mtu mwingine kutekeleza majukumu ya faradhi (wajibu). Kwa hivyo, kwa vile Funga ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Qadhaa yake ni miongoni mwa (Funga za) wajibu, basi hakuna ulazima wala haja ya ruhusa (idhini) ya Mume kwa Mkewe (bali Mke atafunga bila kuomba idhini hiyo), lakini linapokuja suala la Saumu iliyopendekezwa (Saumu ya Mustahabu), akitaka kufunga saumu hiyo ya Mustahabu, anatakiwa kuomba idhini ya Mumewe.
Your Comment