Sambamba na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kuendeleza vita vya kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ghaza na kuzuia kikamilifu misaada ya kibinadamu isiingizwe katika eneo hilo uliloliwekea mzingiro, nchi za Magharibi zinazouunga mkono utawala huo ghasibu hususan Ujerumani na Marekani nazo pia zimeshadidisha mashinikizo na ukandamizaji dhidi ya watetezi na waungaji mkono wa Palestina.
Maandamano ya waungaji mkono wa Palestina nchini Ujerumani
Kuhusiana na suala hilo, serikali ya Ujerumani imeendelea kuchukua hatua za kuzima sauti za wapinzani wa utawala wa Kizayuni na vita vya Ghaza, kwa kuamuru wanaharakati wanne watetezi wa Palestina wahamishwe nchini humo kwa tuhuma za kushiriki katika maandamano. Wakosoaji wa uamuzi huo uliochukuliwa hivi majuzi na serikali ya Berlin wanasema, huo ni muelekeo mpya unaoonyesha jinsi Ujerumani inavyochukizwa na vuguvugu la kuiunga mkono Palestina. Tangu vilipoanza vita dhidi ya Ghaza mnamo Oktoba 2023, mivutano imeshtadi ndani ya Ujerumani kutokana na hatua za viongozi wa nchi hiyo za kupiga marufuku maandamano, kufuta baadhi ya matukio ya mikusanyiko, na vilevile kuamua taasisi za kitamaduni za nchi hiyo kuwatenga wasanii wanaojaribu kuuelimisha umma na kuufanya uwe na uelewa zaidi kuhusu kadhia ya Palestina. Wanaharakati hao watetezi wa Palestina wakiwemo watatu wenye uraia wa nchi za Ulaya na mmoja ambaye ni raia wa Marekani wanatuhumiwa kushiriki katika maandamano mbalimbali nchini Ujerumani ya kuwaunga mkono wananchi wa Palestina. Timu ya mawakili wanaowatetea wanaharakati hao inasema, mashtaka yaliyofunguliwa dhidi yao ni kisingizio tu cha kukandamiza uhuru wa kutoa maoni ya kisiasa na kufanya maandamano na mikusanyiko hususan ya kuunga mkono Palestina. Amri ya kuwafukuza wanaharakati hao imetolewa wakati Ujerumani inashutumiwa kwa ukandamizaji mkubwa inaofanya dhidi ya wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina.
Ujerumani, ambayo ni muuzaji wa pili mkubwa wa silaha kwa Israel baada ya Marekani, imekuwa kila mara ikiunga mkono na kutoa kauli za kutetea na kuhalalisha jinai zinazofanywa na utawala huo wa Kizayuni huko Ghaza. Katika muda wote wa vita vya Ghaza, vilivyoanza baada ya Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa iliyotekelezwa Oktoba 7, 2023, na ambavyo hadi sasa vimepelekea kuuawa shahidi zaidi ya watu 50,000, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake, viongozi wa Ujerumani, hususan Kansela wa nchi hiyo Olaf Schulz, wamekuwa kila mara wakitetea mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni kwa kisingizio kuwa ni hatua ya kujihami. Kwa uungaji mkono kamili wa kisiasa na kijeshi unaopata kwa Marekani na Ujerumani, utawala wa Kizayuni umehisi umefunguliwa njia ya kufanya jinai na mauaji ya kimbari ambayo hayajawahi kushuhudiwa dhidi ya Wapalestina wa Ghaza, bila kujali hata chembe miito inayotolewa kimataifa ya kuutaka usimamishe mashambulizi yake hayo ya kikatili na kinyama.
Mbali na hayo, Ujerumani imechukua hatua nyingine ya kuunga mkono utawala wa Kizayuni, ambapo mnamo mwezi Januari 2024 ilijitokeza kupinga mashtaka yaliyofunguliwa dhidi ya utawala wa Kizayuni ya kufanya mauaji ya kimbari huko Ghaza na ikatangaza kuwa iko tayari kushiriki katika vikao vya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ ikiwa mhusika wa tatu wa kutoa ufafanuzi wa Mkataba wa Mauaji ya Kimbari wa mwaka 1948. Berlin inaamini kuwa, kwa kuuunga mkono utawala wa Kizayuni muuaji wa watoto, inaweza kuzuia utawala huo wa kinyama usihukumiwe na Mahakama ya ICJ. Hata hivyo, ukweli ambao Ujerumani haiwezi kuupuuza ni kuzidi kuporomoka nafasi ya utawala wa Kizayuni katika uga wa kimataifa na kuzidi kuongezeka chuki za walimwengu dhidi ya utawala huo ghasibu. Hivi sasa Ujerumani imechukua hatua nyingine katika kuuunga mkono utawala wa Kizayuni kwa kutoa mashinikizo na mbinyo sambamba na kuwakandamiza na kuwafukuza nchini humo watetezi na waungaji mkono wa Palestina. Katika miaka ya karibuni, viongozi wa Berlin wamepiga marufuku maandamano ya kuunga mkono Palestina na kutoruhusu utumiaji wa nembo zinazohusiana na utambulisho wa Palestina.
Katika upande mwingine, nchini Marekani, serikali ya Trump ambayo ina rekodi ndefu ya kuiunga mkono Israel bila masharti wala mpaka wowote, imechukua hatua mpya za kuwakandamiza watetezi wa Palestina na kushadidisha mashinikizo dhidi ya vyuo vikuu ambavyo vimekuwa uwanja wa maandamano na mikusanyiko ya kuwaunga mkono watu wa Ghaza na kulaani jinai za utawala huo wa Kizayuni. Ikulu ya White House imetangaza kupitia taarifa kwamba imezuia zaidi ya dola bilioni 2.2 za msaada wa fedha, pamoja na kandarasi zenye thamani ya dola milioni 60 kwa Chuo Kikuu cha Harvard kutokana na viongozi wa chuo hicho kukataa kutekeleza matakwa ya serikali hiyo. Kabla ya hapo, serikali ya Trump ilituma barua kwa Chuo Kikuu cha Harvard kukitaka kifanye mageuzi makubwa katika mfumo wa uendeshaji, mabadiliko katika sera za udahili wa wanafunzi, kuweka mipaka ya kuasisi jumuiya za wanachuo na wigo wa shughuli zao katika eneo la chuo kikuu. Katika barua hiyo, viongozi wa Chuo Kikuu cha Harvard walionywa pia kwamba ikiwa hawatotekeleza matakwa yaliyoainishwa kwenye barua hiyo, jumla ya dola bilioni tisa za ruzuku ya serikali na kandarasi za chuo hicho zitakuwa hatarini kusimamishwa. Rais wa Chuo Kikuu cha Harvard Alan Karber alitangaza Jumatatu iliyopita kwamba chuo hicho hakitakubali kutekeleza matakwa ya serikali ya Trump.
Trump amewaita waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina kwenye vyuo vikuu vya Marekani kuwa eti ni "wafanya fujo wanaolipwa fedha," akidai kwamba wengi wao si wanafunzi bali ni wafanya fujo wanaopatiwa fedha kwa ajili ya kufanya vitendo hivyo; na akasisitiza kwa kusema: "tutawapata, tutawakamata na kuwafukuza nchini ili wasirudi tena hapa". Kabla ya hapo, rais huyo wa Marekani aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii uitwao Truth Social kwamba bajeti yote ya serikali ya shirikisho kwa chuo, skuli au chuo kikuu chochote kile kinachoruhusu kufanywa maandamano haramu itasitishwa.
Kutokana na ushawishi mkubwa zilionao lobi za Wazayuni ndani ya Marekani na namna serikali na bunge la nchi hiyo la Kongresi zinavyotiwa shemere na kuburuzwa na utawala wa Kizayuni, hatua na harakati yoyote ya kupinga uzayuni, kuwaunga mkono Wapalestina wanaodhulumiwa, na kuwatetea watu wa Ghaza, yakiwemo maandamano na mikusanyiko inayofanywa katika vyuo vikuu, vinahesabiwa kuwa ni dhambi isiyosameheka na kuchukuliwa hatua kali. Kwa kuingia tena madarakani Donald Trump, mwenendo wa kuwakandamiza watetezi wa Palestina nchini Marekani umeongezeka maradufu, na hatua kama vile kuwakamata na kuwafukuza wanachuo, pamoja na kukata misaada kwa vyuo vikuu ambavyo vimekuwa uwanja wa harakati za kupinga Uzayuni, vimekuwa sehemu ya ajenda maalumu za utekelezaji za serikali ya Trump…/
342/
Your Comment