Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA - Sayyidat Fatima Maasoumeh (sa) ni mmoja wa wanawake mashuhuri na watukufu katika historia ya Kiislamu, hasa katika madhehebu ya Shia Ithna’asheri. Alizaliwa tarehe 1 Dhul Qa’adah mwaka 173 Hijria katika mji mtakatifu wa Madina. Yeye ni binti wa Imam Musa al-Kadhim (as), Imamu wa saba katika mlolongo wa Maimamu wa Ahlul Bayt (as), na dada wa Imam Ali al-Ridha (as), Imamu wa nane.
Mama yake alikuwa mwanamke mtukufu aliyejulikana kwa jina la Najma, ambaye pia ni mama wa Imam Ridha (as), jambo linalomfanya Fatima Maasoumeh na Imam Ridha kuwa ndugu wa baba na mama mmoja. Alilelewa katika nyumba ya elimu, uchamungu, na ucha Mungu, akapata malezi bora ya kiroho, kielimu na kimaadili.
Fatima Maasoumeh (sa) alikuwa mashuhuri kwa elimu yake, ibada, na ufasaha. Alifuatilia harakati za kaka yake, Imam Ridha (as), na alikuwa mstari wa mbele katika kutetea haki na kufichua dhulma za watawala wa wakati huo. Katika safari yake ya kuelekea Khurasan kumtembelea kaka yake aliyehamishwa kwa nguvu na Khalifa Ma’mun, Sayyidat Fatima alifika mji wa Qom (Iran ya leo), ambako alipata maradhi mazito na kufariki dunia tarehe 10 Rabi'ul Thani mwaka 201 Hijria. Alizikwa mjini Qom, ambao baadaye ukawa kituo muhimu cha elimu ya Kiislamu.
Kuzaliwa kwa Sayyidat Fatima Maasoumeh (sa) ni tukio lenye baraka kubwa kwa Waislamu, hasa Mashia. Siku hii huadhimishwa kwa shangwe, dua, na kumkumbuka mchango wake katika kulinda mafundisho ya Ahlul Bayt (as). Mwanamke huyu amepewa cheo cha juu na Maimamu, ambapo Imam Ridha (as) alisema: "Yeyote atakayemzuru Maasoumeh Qom, atapata Pepo."
Katika zama hizi, kaburi lake limekuwa mahali pa kumbukumbu, dua, na maarifa, ambapo wanafunzi wa Dini kutoka duniani kote hujifunza katika mji huo.
Hitimisho:
Sayyidat Fatima Maasoumeh (sa) ni mfano bora wa Mwanamke wa Kiislamu: Alikuwa Mcha Mungu, Mjuzi, Mwenye msimamo, na mpenzi wa haki na uadilifu. Maisha yake yote ni mwanga kwa Wanawake wa kila zama, na kumbukumbu ya kuzaliwa kwake ni fursa ya kumkumbuka, kuhuisha, na kuiga maisha yake.
Your Comment