Shirika la Habari la Tasnim limenukuu makala iliyoandikwa na gazeti la habari za kiuchumi la Calcalist la Israel ikisema kwamba mabilioni ya dola za India yaliyomiminwa kwenye viwanda vya silaha vya Israel kupitia ununuzi wa silaha kama makombora na ndege zisizo na rubani, zenye thamani ya dola bilioni kadhaa, katika miaka iliyopita, yamechangia pakubwa kwenye vita vya hivi karibuni kati ya India na Pakistan.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa: Mapigano kati ya majeshi ya India na Pakistan yalikuwa yamehamisha hisia za walimwengu kutoka kwenye jinai na mashambulizi ya Israel dhidi ya Palestina hasa Ghaza yanayoendelea kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa huku makubaliano tete ya kusimamisha vita baina ya nchi hizo mbili yakiwa hayatoi dhamana yoyote ya kutozuka upya mapigano baina ya nchi hizo zinazomiliki silaha za nyuklia na kuzifanya kwa muda fulani hisia za walimwengu zitekwe na vita baina ya India na Pakistan.
Gazeti la Calcalist la Israel limefichua kuwa India imetumia idadi kubwa ya silaha ilizonunua kutoka kwa utawala wa Kizayuni, kushambulia Pakistan.
Licha ya Marekani kutangaza kuwa imezipatanisha India na Pakistan na mapigano yamesimama, lakini jana (Jumapili) nchi hizo mbili ziliendelea kushutumiana kuwa haziheshimu makubaliano hayo. Gazeti hilo la Kizayuni limesema kuwa, kuweko shehena kubwa ya silaha ambazo India imenunua kutoka kwa Israel, kunachangia hali tete iliyopo baina ya nchi hizo mbili jirani za kusini mwa Asia.
Gazeti hilo la Israel limeandika: Moja ya silaha hizo ambazo India imenunua kutoka kwa utawala wa Kizayuni ni mfumo wa silaha za rununu wa "IAI Harop" ambao ni wa droni na ndege isiyo na rubani ya "kujiripua" yenyewe ambayo ina uwezo wa kupaa kilomita mia kadhaa na kubeba mabomu yenye uzito wa takriban kilo 10.
Wachambuzi wa masuala ya silaha za kijeshi wanasema kuwa, ndege hiyo isiyo na rubani ya Israel ina uwezo wa kuruka kwa muda wa takribani saa sita katika mwinuko wa kilomita kadhaa kutoka eneo linalolengwa na inapopokea maagizo kutoka kwa muongozaji wake aliyeko mbali, hukimbia kwa kasi kubwa kuelekea kwenye shabaha iliyokusudiwa na baadaye hujiripua na kuangamiza shabaha hiyo.
Droni ya Harop imetengenezwa na shirika la Israel Aerospace Industries (IAI) M.B.T. kwenye maabara yaliyoko katikati mwa Israel. Hiyo ni moja na droni na matoleo mapya ya ndege zinazojiendesha zenyewe, ambapo matoleo mengine ya droni kama hizo ni Harpy na Mini Harpy ambazo kila moja inagharimu mamia ya maelfu ya dola.
Taarifa zinaonesha kuwa jeshi la India lilianza kununua droni za Harpy za Israel, takriban miaka 15 iliyopita, na katika miaka ya hivi karibuni ununuzi huo umeongezeka sana ukijumuisha kandarasi zenye thamani ya mamia ya mamilioni ya dola. Wimbi la mashambulizi ya kijeshi ya India dhidi ya Kashmir inayosimamiwa na Pakistan hivi karibuni lilijumuisha matumizi ya makumi ya aina hizo za silaha za Israel.
Kwa mujibu wa gazeti la Calcalist, taarifa kutoka Pakistan zinaonyesha kuwa, jeshi la nchi hiyo lilikamata ndege zisizo na rubani kati ya 12 hadi 25 wakati wa mapigano hayo. Taarifa za vyombo vya habari zinaonyesha kuwa zaidi ya ndege 77 za jeshi la India zilitunguliwa na jeshi la Pakistan.
Picha za mabaki ya ndege hizo zisizo na rubani zimechapishwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutunguliwa na jeshi la Pakistan. Nyaraka zilizotolewa wakati vita vilipokuwa vinaendelea zinaonesha kuwa moja ya sehemu za ndege hizo zisizo na rubani zina maelezo ya kampuni iliyotengeneza mfumo mdogo uliowekwa ndani yake, ambayo ni kampuni ya Enercon. Kampuni hiyo inazalisha vifaa vya umeme kwa ajili ya sekta ya ulinzi na hadi hivi karibuni ilikuwa inamilikiwa na mfuko wa Fortissimo ya Israel, lakini iliuzwa mwishoni mwa mwaka jana na kununuliwa na kampuni ya Marekani ya Bell Fuse kwa dola milioni 320.
Mtazamo wa baadhi ya wachambuzi wa mambo ni kwamba, mbali na lengo la kutaka kuhamisha hisia za walimwengu ili zisahau jinai za Israel huko Ghaza, ufichuaji huu wa gazeti la Israel unaonesha kuwa utawala wa Kizayuni unajali maslahi yake binafsi tu na haushughulishwi na maafa ya kibinadamu wanayopata wanadamu wa maeneo tofauti duniani kutokana na silaha zake. Aidha, kuuawa na kujeruhiwa makumi ya watu katika vita vya hivi karibuni baina ya India na Pakistan ambapo ndani yake India ilitumia kwa kiasi kikubwa silaha ilizonunua kutoka kwa Israel, ni ushahidi wa namna utawala wa Kizayuni unavyohatarisha usalama wa dunia nzima.
342/
Your Comment