22 Mei 2025 - 01:45
Nguvu ya Maamuzi Inashinda Haja na Matamanio ya Mwanadamu | Matamanio hukutaka uishi kwa sasa; Maamuzi hukutaka uishi kwa heshima

“Watu wengi wanataka kubadilika katika maisha yao na kuwa na maendeleo mazuri, lakini ni wachache kati yao wanaofanya hivyo, kwa sababu Nguvu ya Maamuzi ndani yao ni ndogo, na ukizingatia Nguvu ya Maamuzi ndio inayobeba matokeo chanya, na si haja pekee.”

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Tuna methali au nukuu yenye maana pana na ya kina inayosema: "Nguvu ya maamuzi Inashinda Haja au Matamanio ya Mwanadamu”. Methali hii au msemo huu au nukuu hii yenye maana pana, inaweza kufasiriwa namna hii kama ifuatavyo:

Uamuzi wa mtu kufanya jambo kwa dhamira thabiti, una nguvu na athari kubwa zaidi kuliko ile hitaji la kawaida au hamu ya jambo hilo.

Maana Kwa Undani:

  • "Haja" ni hitaji au hamu - jambo ambalo mtu anatamani au anahitaji.
  • "Maamuzi" ni mwelekeo wa kivitendo, unaochukuliwa baada ya tafakari au msukumo wa ndani.

Hii inamaanisha kuwa hata kama mtu ana hitaji fulani (kama vile kubadilisha maisha yake ili aweze kupata maendeleo chanya, au kujifunza jambo fulani, au kuacha tabia na mwenendo fulani), hatua halisi na mafanikio hayatategemea tu haja hiyo aliyokuwa nayo, bali itabidi awe na uamuzi wa kweli, wa dhati na wenye kufuatana na vitendo.

Mfano Wa Matumizi:

“Watu wengi wanataka kubadilika katika maisha yao na kuwa na maendeleo mazuri, lakini ni wachache kati yao wanaofanya hivyo, kwa sababu Nguvu ya Maamuzi ndani yao ni ndogo, na ukizingatia Nguvu ya Maamuzi ndio inayobeba matokeo chanya, na si haja pekee.”

Nguvu ya Maamuzi Inashinda Haja na Matamanio ya Mwanadamu | Matamanio hukutaka uishi kwa sasa; Maamuzi hukutaka uishi kwa heshima

Nguvu ya Matamanio na Nguvu ya Maamuzi

Matamanio ni sauti ya mwili. Ni hisia zinazoibuka ndani yetu bila kuomba ruhusa — wakati mwingine kwa ghafla, zenye nguvu, na zisizochoka. Ni haja ya mwili, hitaji la kihisia, au hamu ya kupokea raha ya muda mfupi.

Lakini maamuzi ni sauti ya akili. Ni uamuzi wa kufikiri kabla ya kutenda. Ni uwezo wa kuona mbele — kuchagua maumivu ya muda kwa ajili ya heshima ya kudumu. Ni sauti ya nafsi inayosema:

"Najua naweza, lakini sitaki — kwa sababu najiheshimu."

Katika mapambano haya mawili:

  • Matamanio huchochea tamaa.
  • Maamuzi huchochea thamani.

Mwanamke (au Mwanaume) anapochagua kujizuia licha ya hamu iliyo wazi na halali katika hali fulani, hana budi kupongezwa, si kwa sababu hahisi au hana matamanio, bali kwa sababu (ana nguvu ya maamuzi) kushinda kilicho ndani yake (matamanio).

Kushinda vita vya nje ni ushindi wa kawaida, lakini kushinda vita vya ndani - vya matamanio na tamaa - ni ushindi wa mashujaa.

Nukuu Fupi:

  • “Nguvu ya matamanio huja kwa kasi, lakini nguvu ya maamuzi hudumu na hutoa heshima ya kweli.”
  • “Matamanio hukutaka uishi kwa sasa; maamuzi hukutaka uishi kwa heshima.”

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha