Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Ndugu zangu Waislamu, Hapana Shaka kuwa Sisi Wanadamu wenye Heshima na Karama. Hivi ndivyo tulivyoumbwa na Mwenyezi Mungu.
Vyovyote tunavyoishi na lolote tutakalolifanya katika Maisha yetu, tutalifanya kwa Lengo la kuhifadhi Heshima na Karama yetu kama Wanadamu.
Kwa ibara nyingine: Hatufanyi tunaloamua kulifanya kwa ajili ya maisha yetu kwa sababu ya njaa, wala kiu ya mkate, bali ni kwa sababu ya kiu ya Heshima na Karama ya Mwanadamu.
Kwa mfano: Katika Jamii zetu, kuna watu wanatushawishi kwa maneno mepesi sana kama vile: "Nipeni kura zenu, nitashughulikia - nitashusha - bei ya mkate."
Lakini nawauliza: Je, sisi tunapochagua Kiongozi wetu katika Jamii yetu, maana yake Malengo yetu ni mkate?! Sisi ni watu wa mkate au ni watu wa karama na heshima?!.
Hatuchagui viongozi kwa sababu ya mikate, bali kwa sababu ya mustakabali wa utu wetu na Heshima yetu kama Wanadamu.
Tumeumbwa na Mwenyezi Mungu tukiwa na Heshima, tukiwa bora kuliko viumbe wote, lakini mara nyingi sisi wenyewe ndio tunaochuma mabaya tunayoyapata kupitia mikono yetu wenyewe, pale tunapomsahau Mwenyezi Mungu, na tunapoweka tamaa mbele ya haki.
Na matokeo yake nini?. Hapana shaka kuwa yafuatayo ndio matokeo yake ambapo: Mwenyezi Mungu huwasimamisha juu yetu watu waovu watutawale na sio kutuongoza.
Tunapokosa kusimama kwa haki, tunapoacha kuikemea dhulma, tunapoacha kujitambua - hapo ndipo tunawekwa chini ya utawala wa dhulma kama ilivyokuwa kwa watu wa Fir'aun, aliowadhoofisha, akaondoa heshima yao, na kuwafanya watumwa wa hofu.
Ndugu zangu, Sisi wenyewe ndio suluhisho. Kwa mikono yetu tunaweza kujiletea maangamizi, lakini kwa mikono hiyo hiyo tunaweza kujikomboa.
Sisi ndio tunaweza kusema hapana kwa udhalimu, hapana kwa unyonge, hapana kwa viongozi wasiojali Utu wetu na Heshima yetu.
Lazima tuamke. Lazima tutambue kuwa hatukuzaliwa ili kudhalilishwa.
Lengo letu si mkate - Bali ni kuishi kwa hadhi, kwa karama, kwa ujasiri wa kusimamia ukweli, hata kama ni mchungu.
Tusimame na wanyonge:
Tusisahau ndugu zetu wanaodhulumiwa, kama Wapalestina, ambao kila siku wanapigania si mkate - bali heshima yao, ardhi yao, utu wao na Karama yao.
Kama hatutatetea haki yao, basi tumepoteza haki ya kujiita watu wa Karama na Heshima.
Napenda kusema hivi:
Tutakapoamua, kwa moyo mmoja na kwa imani thabiti, kuwa hatutakubali tena kununuliwa kwa mkate; tutakapoamua kuwa heshima yetu haina bei - basi hapo ndipo tutakapoanza safari ya kweli ya ukombozi wa kiutu, kisiasa, na kiroho.
Mwenyezi Mungu atupe Taufiq na atuongoze.
Was_Salam Alaikum Warahmatullahi Taala wabarakatuh.
Your Comment