Kujiunga Algeria na Benki ya Ustawi Mpya ya BRICS kumeongeza juhudi za jumuiya hiyo za kuunda ulimwengu wa kifedha wa pande kadhaa. Dilma Rousseff, Mkuu wa benki hiyo awali alitangaza mipango ya kubadilisha Benki ya Ustawi Mpya ya BRICS kuwa "taasisi muhimu ya kifedha" kwa nchi zinazoendelea na masoko yanayoibuka. Rousseff ameipongeza Algeria kwa kujiunga na benki hiyo, akisisitiza kuwa itasaidia kuimarisha ushawishi wa kimataifa wa Benki ya Ustawi Mpya ya BRICS.
Benki ya Ustawi Mpya ya BRICS (NDB) ilianzishwa mwaka 2014 na Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. Benki hiyo inakusudia kukusanya rasilimali kwa ajili ya utekelezaji wa miundombinu na miradi ya maendeleo endelevu katika nchi wanachama wa BRICS kupitia utoaji wa mikopo, dhamana na vyombo vingine vya kifedha.
Mohammad Reza Farzin, Gavana wa Benki Kuu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia ametangaza kuwa hivi karibuni Tehran itajiunga na Benki ya Ustawi Mpya ya BRICS.
Uanachama wa Iran na nchi nyingine huru katika benki hiyo utakuwa na taathira nyingi kwa uchumi wa dunia katika nyanja mbalimbali, jambo ambalo bila shaka litaimarisha ushirikiano kati ya nchi zinazoinukia kiuchumi katika ngazi ya kimataifa katika miaka ijayo.
Ili kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na nchi nyingine za Magharibi, Iran inaweza kutoa vyanzo mbadala vya kufadhili miradi ya miundombinu, ikiwa ni pamoja na uchukuzi, nishati na mawasiliano, kwa kujiunga na benki hiyo ya BRICS. Benki hii inatoa mikopo kwa nchi wanachama kwa viwango vinavyokubalika vya faida, jambo ambalo linaweza kuwa mbadala mzuri dhidi ya taasisi za kifedha za Magharibi kama vile Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia.
Nchi wanachama wa benki ya NDB
Suala la msingi na muhimu zaidi kuhusu wanachama wapya wa benki ya NDB ni kuwa watapunguza utegemezi wao kwa mfumo wa kifedha wa kimataifa wa Magharibi unaoegemea kwenye dola na taasisi za kiuchumi chini ya ushawishi wa madola ya kibeberu ya Magharibi. Benki ya NDB, inayoangazia matumizi ya fedha za ndani na kuunda mifumo mbadala ya malipo kama vile kubadilishana fedha zisizo za dola, itasaidia Iran na nchi nyingine wanachama wa kundi hilo kukabiliana na vikwazo.
BRICS inayojumuisha Uchina, Russia, India, Brazili, Afrika Kusini na Iran ina jukumu muhimu katika uchumi wa kimataifa, na Iran inaweza kupanua uhusiano wake wa kiuchumi na nchi hizo kwa kujiunga na NDB. Ushirikiano huu pia utapelekea kuongezeka kwa uwekezaji, uhamisho wa teknolojia na ushirikiano wa viwanda kati ya nchi wanachama.
Benki hii ya BRICS inaangazia miradi ya maendeleo endelevu na nishati ya kijani, ambayo inaendana na malengo ya Iran ya kujikita katika uzalishaji wa nishati safi na usiotumia mafuta na hivyo kupunguza utegemezi wa mafuta katika kudhamini mapatano ya taifa. Iran inaweza kuvutia uwekezaji wa kifedha katika miradi ya jua, upepo na umeme unaotokana na maji kwa njia hii.
Uanachama katika NDB pia unaipa Iran fursa ya kuwa na nafasi muhimu katika kambi ya kiuchumi isiyo ya Magharibi na hivyo kuimarisha nafasi yake kama mhusika mkuu katika ushirikiano wa Kusini-Kusini. Suala hili ni muhimu hasa katika muktadha wa ushirikiano wa kimkakati na China na Russia.
Kwa kuzingatia uwanachama wa nchi zenye ushawishi katika BRICS, zikiwemo Iran, Uchina na Russia, ambazo zina jukumu kubwa katika soko la kiuchumi la kimataifa, Benki ya Ustawi Mpya ya BRICS pia itakuwa na nyenzo tofauti za kifedha katika suala zima la kuvutia uwekezaji na uwezo wa kifedha kutoka nchi wanachama.
Kuundwa na kuendelezwa shughuli za benki hii kutahimiza nchi mbalimbali kushirikiana na BRICS na hivyo kuliweka kundi hili na taasisi yake ya kifedha katika nafasi nzuri zaidi ikilinganishwa na mashirika mengine ya kifedha yanayoungwa mkono na nchi za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa. Umuhimu wa ushirikiano kati ya Iran na nchi wanachama wa BRICS utasaidia kwa namna fulani kuunda soko kubwa la kiuchumi katika ngazi ya kimataifa bila ya kuihitajia Marekani na nchi nyingine za Magharibi, ambapo wanachama wote wa kundi hili wanakubaliana na suala hilo.
Your Comment