Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Katika tukio la kipekee lililowakusanya waumini wa dini ya Kiislamu kutoka maeneo mbalimbali, Jukwaa la Qur'an Tukufu Jijini Tanga lilipambwa kwa umaridadi katika Uwanja wa Michezo wa Mkwakwani – Tanga, huku likibeba nembo za taasisi kubwa za Kiislamu na zingine zisizokuwa za Kiislamu ambazo kwa pamoja ziliunganisha nguvu, umoja na mshikamano na Ushirikiano kwa ajili ya tukio hilo adhimu la Qur'an Tukufu, chini ya kaulimbiu: "Qur'an Inatuunganisha".
Taasisi zilizoshiriki kwa dhati katika maandalizi na utekelezaji wa Kongamano hili ni:
1_Jamiat Al-Mustafa (s) International University – Tawi la Tanzania
2_Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)
3_Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT)
4_Kitengo cha Utamaduni wa Iran.
Katika kilele cha hafla hii, waumini walipata fursa ya kipekee ya kusikiliza wasomaji bingwa wa Qur'an kutoka Iran - kama ifuatavyo: Ustadh Shakernejad, Ustadh Abolghasemi, Qari kijana Mohammad Hossein Azimi, na Muhanna Ghanbari – ambaye ni mhifadhi wa Qur’an nzima.
Wasomaji hawa walionyesha Ustadi mkubwa katika kusoma Quran, wakiongozwa na Mwamba wa Tajweed, Ustadhi Shakirnajad, ambaye aliteka nyoyo za hadhira kwa sauti yake ya kuvutia na usomaji ulioshika Ahkam zote za Tajwidi kwa ustadi mkubwa.
Tanzania pia haikubaki nyuma, ambapo Sheikh Rajai na Anko Idi walionyesha umahiri wao katika Usomaji wa Qur'an na kuzikonga nyoyo za wasikilizaji. Kwa hakika walitoa mchango wao mkubwa kwa kusoma Qur'an kwa lahani za kipekee zilizoonesha hazina ya vipaji vya ndani ya nchi.
Mapokezi Chanya na Athari kwa Jamii
Wadau mbalimbali wamepongeza kwa dhati ushirikiano huu wa maridhawa uliowezesha waumini wengi kupata furaha ya nyoyo kwa kushiriki kongamano hili. Washiriki waliguswa sana na namna usomaji wa Qur'an ulivyopangwa, kuwasilishwa, na kuhifadhi ladha ya usomaji kutoka madhehebu mbalimbali kwa kuheshimu misingi ya umoja na amani.
Tumekuwekea video fupi ya tukio hili adhimu ili upate kuona jinsi lilivyofanikiwa kwa kiwango cha juu na kuacha athari chanya katika nyoyo za waumini na wageni wote waliokuwa sehemu ya Kongamano hili la Kihistoria.
Your Comment