Kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) - ABNA- Leo Jumapili, tarehe 25/05/2025, hafla ya kuvutia ilifanyika katika uwanja wa Mnazi Mmoja, Jijini Dar-es-salaam - Tanzania ikihudhuriwa na watazamaji wengi zaidi Elfu Kumi (10) kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar-es-salaam na nje yake, kwa ajili ya kuja kusikiliza wasomaji bingwa na maarufu wa Qur’an Tukufu walioifanya programu hii ya Mahfali ya Qur'an kupendeza kwa visomo vyao vizuri vya Qur'an kwa Njia ya Tajweed.
Hafla hii iliandaliwa kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Al-Mustafa na Ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na Ofisi ya Ushauri wa kiutamaduni wa Iran nchini Tanzania.
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ni Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mshauri wa masuala ya kiutamaduni, na Mwakilishi wa Kikanda wa Jamiat Al-Mustafa (s) nchini Tanzania.
Hafla hii ilifanyika chini ya kauli mbiu ya kuleta umoja isemayo: “Qur’an Inatuunganisha”, na ilipokelewa kwa hamasa kubwa na Wananchi wa Jiji la Dar-es-salaam.
Wadau mbalimbali wa Qur'an Tukufu wametoa shukrani zao maalumu kwa Iran kwa kuleta wasomaji mahiri wa Qur’an nchini Tanzania, wakilitaja tukio hilo kuwa ni ishara ya uhusiano wa kina wa kitamaduni na kidini kati ya Mataifa haya mawili.
Katika hafla hii Tukufu ya Qur’an, wasomaji wa Kiirani walioshiriki ni pamoja na Ustadh Shakernejad, Ustadh Abolghasemi, Qari kijana Mohammad Hossein Azimi, na Muhanna Ghanbari - ambaye ni mhifadhi wa Qur’an nzima.
Wasomaji hawa wa Qur'an Tukufu, walitumbuiza kwa tilawa za kuvutia ambazo zilijaza kumbi za viwanja vya Mnazi Mmoja hali ya furaha ya kiroho.
Aidha, baadhi ya wasomaji wa Kitanzania pia walipata nafasi ya kusoma Qur’an na walipokelewa vyema na hadhira.
Your Comment