Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa kauli hiyo leo jioni katika ujumbe kwa njia ya televisheni ya taifa ya Iran ambapo amepongeza mienendo thabiti ya kijasiri na ya kutambua wakati ya taifa la Iran katika kadhia ya hivi karibuni ya uchokozi wa kipumbavu na kikhabithi wa adui Mzayuni. Amesisitiza kwamba sifa hizo za taifa la Iran ni ishara ya ukomavu wa kiakili na kiroho. Ameongeza kuwa taifa la Iran litasimama kidete kukabiliana na vita vya kulazimishwa kama ambavyo litasimama kidete dhidi ya amani ya kutwishwa.
Imama Khamenei pia ameashiria matamshi ya vitisho na ya kijinga ya rais wa Marekani na kuongeza kuwa: “Watu wenye akili na busara ambao wanaifahamu Iran, taifa na historia ya Iran wanaelewa vyema kwamba katu hawapaswi kuzungumza na taifa hili kwa lugha ya vitisho kwani taifa la Iran halisalimu amri. Wamarekani wafahamu kuwa kuingia katika vita vyovyote vya kijeshi bila shaka kutawapelekea kupata kipigo ambacho hakiwezi kufidiwa.”
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amepongeza harakati adhimu ya taifa la Iran katika matembezi ya Siku ya Ghadir na pia mijumuiko na maandamano ya siku za hivi karibuni hasa baaada ya Swala ya Ijumaa. Aidha amepongeza harakati nzuri na iliyojaa maana ya kimaanawi ya mtangazaji mwamnamke wa televisheni wakati jengo alimokuwa akirusha matangazo mubashara liliposhambuliwa na utawala wa Kizayuni na kusema: “Hatua yake ya kutamka Takbir ni ishara ya nguvu za taifa la Iran ambayo iliwasilishwa kwa ulimwengu mzima na ni tukio la kihistoria na lenye thamani kubwa.”
Ayatullah Khamenei amesema nukta nyengine muhimu ni kuwa, uvamizi wa kijinga na wa kikhabithi wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran ulijiri wakati maafisa wa serikali ya Iran walikuwa wanashiriki katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani. Amesema kwamba upande wa Iran hakudhani kungekuwa na hatua ya ghafla ya kijeshi na kuongeza kuwa: “Tokea mwanzo kulikuwa na hisia kuwa Marekani ilikuwa inatekeleza njama chafu kwa niaba ya utawala wa Kizayuni na kwa kuzingatia matamshi ya karibuni ya maafisa wa Marekani, hisia hiyo ilipata nguvu siku baada ya siku.”
Imam Khamenei amesema taifa la Iran litasimama kidete dhidi ya vita vya kulazimishwa, kama ambavyo daima limekuwa likifanya hivyo. Aidha amesema taifa la Iran linapinga amani ya kutwishwa na halitasalimu amri kutokana na mashinikizo.
Ayatullah Khamenei amesema utawala wa Kizayuni umefanya kosa kubwa na umetenda jinai nzito na lazima uadhibiwe na unaendelea kuadhibiwa hivi sasa. “Adhabu inayotekelezwa na taifa la Iran na majeshi yetu, na ambayo inapangwa siku za usoni dhidi adui huyo wa kieshetani ni adhabu kali ambayo tayari imewadhoofisha. Ukweli kuwa rafiki yake, yaani Muamerika ameingia katika medani na kutoa matamshi anayotoa ni ishara kuwa utawala huo umedhoofika na haujiwezi.”
Ayatullah Khamenei amesema: Nukta ya mwisho ni kuwa rais wa Marekani sasa anatoa vitisho dhidi yetu. Si tu kuwa anatoa vitisho, bali pia anatumia lugha chafu isiyokubalika kwa kutangaza wazi wazi kuwa taifa la Iran linapaswa kusalimu amri mbele yake. Wakati mtu anapotoa matamshii kama hayo, kwa kweli ni jambo la kushangaza. Kwanza , wanapaswa kutoa vitisho kama hivyo kwa wale ambao wanaogopa vitisho. Taifa Ia Iran halitishiki kwa vitisho kama hivyo. “Msidhoofike wala msihuzunike, mtapata ushindi iwapo mna imani.”(Qur’ani Tukufu 3:139). Taifa la Iran lina imani ya dhati kuhusu aya hii na hivyo vitisho haviathiri misimamo ya taifa hili.”
Ayatullah Khamenei ametoa wito kwa taifa la Iran kuzingatia aya hiyo daima na kuongeza kuwa:”Alhamdulillah, maisha yanaendelea kama kawaida, msimfanye adui ahisi kuwa mnamuogopa au mnajihisi dhaifu mbele yake. Adui akihisi unaogopa, hatakuacha. Endeleeni kwa nguvu ambayo munaonyesha leo.”
Kiongozi Muadhamu amehitimisha ujumbe wake kwa kusema: “Na Ushindi unatoka kwa Mwenyezi Mungu pekee, Mwenye Adhama na Mwenye Hekima.” (Qur’ani 3;126) Msiwe na shaka kuwa, kwa yakini, Mwenyezi atalipa taifa la Iran ushindi, huu utakuwa ni ushindi wa haki na ushindi kwa uapnde ambao uko katika njia ya haki, Inshallah.
342/
Your Comment