25 Oktoba 2025 - 21:37
Source: Parstoday
Marekani yatuma meli kubwa zaidi ya kivita Amerika ya Kusini; Venezuela yatabiri hatari kubwa

Marekani imeamua kutuma meli ya kivita ya kubeba ndege, USS Gerald R. Ford , ambayo ndiyo kubwa zaidi duniani,  pamoja na meli zingine tano za kivita kwenda Amerika ya Kusini, hatua ambayo imekosolewa vikali na Venezuela ikiitaja kuwa ya kichokozi, hatarishi, na kinyume cha sheria za kimataifa.

Hatua hiyo, inayotajwa kuwa miongoni mwa maandalizi makubwa zaidi ya kijeshi ya Marekani katika eneo hilo kwa miongo kadhaa, ilitangazwa Ijumaa na msemaji wa Wizara ya Vita ya Marekani, Pentagon.

Afisa huyo alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za “kugundua, kufuatilia, na kudhibiti wahusika na shughuli zisizo halali.”

Hata hivyo, uamuzi huo umeibua hofu ya uwezekano wa jaribio la kuleta machafuko au hata uvamizi wa moja kwa moja dhidi ya Venezuela kwa kutumia visingizio visivyo na msingi.

Wachambuzi na waangalizi wa kimataifa wameonya kuwa ukubwa wa oparesheni hiyo unazidi kwa kiasi kikubwa operesheni za kawaida za kupambana na dawa za kulevya.

Kikosi cha mashambulizi cha Gerald Ford kinatarajiwa kuungana na takriban wanamaji na wanajeshi 6,000 wa Marekani walioko tayari kwenye meli nane katika eneo hilo, hatua itakayofikisha jumla ya askari wa Marekani katika ukanda huo hadi  zaidi ya 10,000.

Kuzidi kwa hali hii kunafuatia kauli ya hivi karibuni ya Donald Trump, aliyekiri kuidhinisha operesheni za shirika la kijasusi la CIA ndani ya Venezuela na kwamba alikuwa “anatafakari mashambulizi ya nchi kavu.”

Rais huyo wa Marekani amekuwa akitoa madai yasiyo na ushahidi kwamba serikali ya Rais Nicolás Maduro inahusiana na makundi ya kihalifu yanayodaiwa “kuivamia” Marekani kupitia biashara ya dawa za kulevya na uhamiaji haramu, madai ambayo yamekanushwa mara kwa mara na mashirika ya kimataifa na hata tathmini za kijasusi za Marekani yenyewe.

Tangu Septemba, Washington imeendesha mashambulizi kadhaa dhidi ya meli za kiraia na za uvuvi katika Bahari ya Karibiani, ikidai zinahusiana na biashara ya dawa za kulevya bila kutoa ushahidi wowote.

Kwa mujibu wa maafisa wa Umoja wa Mataifa na wataalamu wa sheria za kimataifa, mashambulizi hayo yanakiuka sheria za Marekani na zile za kimataifa, na yanachukuliwa kama mauaji nje ya mfumo wa kisheria.

Mamlaka za Venezuela zimesisitiza kuwa zitalinda kwa uhuru na mipaka ya taifa hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Venezuela Vladimir Padrino ameitaja hatua ya sasa ya Marekani kuwa “tishio kubwa zaidi la kijeshi katika kipindi cha miaka 100 iliyopita,” huku akisisitiza azma ya Caracas ya kudumisha amani na akaonya kwamba Venezuela haitavumilia aina yoyote ya uchokozi.

Your Comment

You are replying to: .
captcha