21 Desemba 2025 - 11:31
Mamilioni ya Wayemeni Wafurika Barabarani Kuitetea Qur’ani Tukufu Baada ya Kudharauliwa Nchini Marekani

Qur’ani Tukufu ni Kitabu Kitakatifu kisichoguswa, na kitendo chochote cha kuidharau kitapokelewa kwa upinzani na laana kali kutoka kwa Waislamu duniani kote.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Tarehe 19 Disemba 2025, Jamhuri ya Yemen ilishuhudia maandamano makubwa ya kihistoria, baada ya zaidi ya Wayemeni milioni kumi kujitokeza kwa wingi katika miji mbalimbali kote nchini, wakionesha hasira kali na kulaani kitendo cha mgombea wa kisiasa wa Marekani aliyeteketeza Qur’ani Tukufu.


Katika mji mkuu Sana’a, mandhari ilikuwa ya kipekee na yenye hisia nzito, ambapo zaidi ya nakala milioni mbili za Qur’ani Tukufu ziliinuliwa juu na waandamanaji, kama ishara ya mshikamano, mapenzi na utetezi wa Kitabu Kitakatifu cha Uislamu. Waandamanaji walipaza sauti zao kwa kauli mbiu zilizothibitisha kuwa Qur’ani ni heshima na mstari mwekundu kwa Waislamu wote duniani.


Maandamano hayo yalifanyika kwa amani lakini kwa wingi mkubwa, yakihusisha miji mingi ikiwemo Sana’a, Saada, Hodeidah, Dhamar, Ibb na Taiz, ambapo wananchi walikusanyika katika viwanja vikuu, wakiwa wamebeba Qur’ani, mabango na maandishi yaliyolaani Uislamu kuchukiwa (Islamophobia) na kudai kuheshimiwa kwa alama na misingi ya dini.


Viongozi wa dini, wanazuoni na wazee wa kijamii walitoa hotuba mbele ya waandamanaji, wakisisitiza kuwa kudharau Qur’ani Tukufu si uhuru wa kujieleza bali ni kitendo cha chuki kinachoumia hisia za zaidi ya Waislamu bilioni moja duniani. Walionya kuwa vitendo kama hivyo vinaongeza chuki, mgawanyiko na hatari ya migogoro ya kimataifa.


Maandamano haya makubwa yalionesha msimamo wa pamoja wa wananchi wa Yemen, bila kujali tofauti za kisiasa au kijamii, katika kutetea utukufu wa Qur’ani Tukufu. Waandamanaji pia walitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti za kisheria kuzuia kurudiwa kwa vitendo vya kudhalilisha vitabu vitakatifu na dini.


Kwa ujumla, ujumbe wa Wayemeni ulikuwa wazi na thabiti: Qur’ani Tukufu ni Kitabu Kitakatifu kisichoguswa, na kitendo chochote cha kuidharau kitapokelewa kwa upinzani na laana kali kutoka kwa Waislamu duniani kote.

Mamilioni ya Wayemeni Wafurika Barabarani Kuitetea Qur’ani Tukufu Baada ya Kudharauliwa Nchini Marekani

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha