21 Desemba 2025 - 14:06
Usijivune kwa Maneno Maneno na Kujiona Mwenye Fadhila | Ibada na Jema lolote bila Unyenyekevu, ni Njia ya kupoteza kila Kheri

Baadhi ya Mabedui walikuwa wakimfanyia Mtume (s.a.w.a) madai ya fadhila kwa kusilimu kwao, kama Qur’ani inavyosema: “Wanakuonea fadhila kwa kusilimu kwao.” Basi Qur’ani ikawafunza adabu kwa kusema: “Sema: Msinionee fadhila kwa Uislamu wenu; bali Allah ndiye anayekuoneeni fadhila kwa kuwaongoza kwenye imani, ikiwa nyinyi ni wakweli.” (Al-Hujurāt: 17).

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Ifuatayo ni Nasaha kutoka kwa Samahat Sheikh Dr.Talal Al-Hassan - ambapo anasema: Usijione Mwenye Fadhila (kwa watu, na kujigamba au kujivuna kwa Maneno Maneno)! Mara nyingi mtu hujivunia sana matendo yake mema, akisema moyoni au waziwazi: “Nimefanya hivi, nimetimiza vile”, hadi huona ubora wa kazi yake kuwa mkubwa sana mbele ya nafsi yake.

Wakati mwingine hali hii ya kujiridhisha kupita kiasi (‘ujbu) humfanya hata aanze kutarajia au kudai asifiwe na watu kwa matendo yake.
Na pale ‘ujbu unapopuuzwa bila kutibiwa, huendelea kukua na kugeuka ugonjwa hatari zaidi: kujiona mwenye haki ya kuwafanyia watu hisani. Hapo mtu huanza kuona kuwa amewafanyia wengine fadhila, na wakati mwingine huenda mbali zaidi akajiona kana kwamba anamfanyia Allah Subhanahu wa Ta‘ala fadhila, akijiambia: “Nimeswali kiasi hiki, nimefunga kiasi hiki, nimehiji na nimeumra mara kadhaa!” - kauli ambazo ndani yake zimejificha madai ya fadhila kwa Mwenyezi Mungu.
Ilhali, Allah peke Yake ndiye Mwenye fadhila zote, na jambo baya zaidi kabisa ni pale mtu anapodai fadhila kwa Mola wake; hilo ni ujinga na ukosefu mkubwa wa adabu.
Kwa hakika, kisima kile cha giza na kina kirefu - yaani ‘ujbu - huzima kila nuru inayotokana na matendo mema. Na yule nyoka mwenye madoadoa - yaani kujipamba kwa matendo mbele ya nafsi—humeza kila ukamilifu unaotokana na amali njema. Badala ya mtu kupata ongezeko la thawabu na ukamilifu, huzama katika upotevu wa giza la ‘ujbu; taa za matendo huzimika, na giza la njia huongezeka.
Baadhi ya Mabedui walikuwa wakimfanyia Mtume (s.a.w.a) madai ya fadhila kwa kusilimu kwao, kama Qur’ani inavyosema:
“Wanakuonea fadhila kwa kusilimu kwao.”
Basi Qur’ani ikawafunza adabu kwa kusema:
Sema: Msinionee fadhila kwa Uislamu wenu; bali Allah ndiye anayekuoneeni fadhila kwa kuwaongoza kwenye imani, ikiwa nyinyi ni wakweli.” (Al-Hujurāt: 17)

Kwa kuhitimisha:
Ikiwa tumefanya jambo jema lolote, basi ni kwa Taufiki ya Allah. Je, inawezekanaje tumfanyie Yeye madai ya fadhila kwa kile alichotuwezesha kukifanya?!. Miongoni mwa alama za imani ya kweli ni kuona kuwa fadhila zote ni za Allah juu yetu katika kila jambo.
Ewe Allah, tupe taufiki ya kuwa na adabu mbele Yako; tusikufanyie madai ya fadhila wala viumbe Wako—si kwa maneno wala kwa matendo—hata kama matendo hayo ni mema.

Usijivune kwa Maneno Maneno na Kujiona Mwenye Fadhila | Ibada na Jema lolote bila Unyenyekevu, ni Njia ya kupoteza kila Kheri

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha