Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Maandamano ya kitaifa ya 22 Bahman (11 Feb) yaliyoandaliwa kuadhimisha miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, yamepata mwangwi mkubwa katika vyombo mbalimbali vya habari vya Kiarabu.
Vyombo hivyo vimeripoti kwa upana ushiriki mkubwa wa wananchi wa Iran katika mji mkuu Tehran pamoja na zaidi ya miji na majiji 1200 nchini kote, wakionyesha mshikamano wao na misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Mitandao ya habari kama Al-Mayadeen, Al-Manar na Al-Masirah, pamoja na magazeti ya Ra’i Al-Youm na Al-Arabi Al-Jadeed, yalieleza kuwa maandamano hayo yalishuhudia ushiriki wa maelfu ya wananchi kutoka matabaka mbalimbali ya jamii, pamoja na kuhudhuria kwa viongozi waandamizi wa kisiasa na kijeshi wa Iran.
Vyombo hivyo pia viliripoti hotuba ya Rais wa Iran, aliyesisitiza umuhimu wa kuendeleza uhusiano wa karibu na nchi jirani, kuimarisha diplomasia ya kikanda, na kulinda maslahi ya taifa la Iran katika mazingira ya changamoto za kimataifa.
Aidha, katika viwanja vya Azadi Square, baadhi ya mafanikio ya kijeshi ya Iran yalioneshwa hadharani kama sehemu ya maadhimisho hayo, jambo lililotajwa na vyombo vya habari vya Kiarabu kuwa ni ujumbe wa uwezo wa Iran katika kulinda uhuru na usalama wake.
Kwa mujibu wa ripoti hizo, hafla ya 22 Bahman ilitafsiriwa kama ishara ya kuhuisha upya ahadi ya wananchi wa Iran kwa malengo, misingi na maadili ya Mapinduzi ya Kiislamu, pamoja na kuonesha mshikamano wa kitaifa dhidi ya shinikizo na vitisho vya nje.
Vyombo vya habari vya Kiarabu vimehitimisha kuwa ushiriki huo mkubwa wa wananchi unaakisi uimara wa mfumo wa Kiislamu wa Iran na kuendelea kwa uungwaji mkono wa watu wake kwa uongozi wa nchi hiyo.
Your Comment