1 Januari 2026 - 22:52
Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran lafichua mafanikio matatu makubwa ya nyuklia

Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran limetangaza mafanikio matatu makubwa ya nyuklia: kuzindua kichochezi cha kwanza cha viwandani kilichotengenezwa ndani ya nchi, kuanza uzalishaji wa hali ya juu wa Carbon-13, na kurejesha cyclotron kwa ajili ya uzalishaji wa dawa za mionzi licha ya vikwazo.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) limetangaza kusajili mafanikio matatu mapya muhimu ya nyuklia, yakiwemo kuzinduliwa kwa kichochezi (accelerator) cha kwanza cha viwandani kilichotengenezwa kikamilifu ndani ya nchi, kuanza kwa uzalishaji wa hali ya juu wa Carbon-13, pamoja na kurejeshwa kazini kwa cyclotron kwa ajili ya uzalishaji wa dawa za mionzi (radiopharmaceuticals).

Tangazo hilo lilitolewa Jumanne na Behrouz Kamalvandi, msemaji wa AEOI, baada ya kushiriki kikao cha Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Bunge la Iran, ambako aliwapa wabunge taarifa kuhusu shughuli za hivi karibuni za shirika hilo.


Jana tu, mafanikio matatu ya msingi yalisajiliwa na shirika. Kwa mara ya kwanza, kichochezi cha viwandani kimezinduliwa nchini, chenye matumizi mbalimbali katika ulinzi wa mazingira, tiba, teknolojia ya nyuklia na utafiti wa kisayansi,” Kamalvandi aliwaambia waandishi wa habari baada ya kikao hicho.


Alieleza kuwa kichochezi hicho ni cha ndani kikamilifu, kimebuniwa na kutengenezwa na wataalamu wa Iran katika kipindi cha miaka minne, na kimeanza rasmi kufanya kazi wiki hii.


Msemaji huyo pia alisifu kuanza kwa uzalishaji wa hali ya juu wa isotopu ya Carbon-13, uliotekelezwa kupitia ufungaji wa mnara wa mita 12 katika kiwango cha nusu-viwanda. Isotopu hiyo ina matumizi mapana katika tiba, sayansi ya nyuklia, dawa za mionzi, viwanda mbalimbali na tafiti za mazingira.


Aidha, Kamalvandi alitangaza kurejeshwa kwa mafanikio kwa cyclotron ambayo ilikuwa imesimama kwa karibu miaka miwili, kutokana na vikwazo vilivyokwamisha uingizaji wa vifaa muhimu.


“Licha ya kutopatikana kwa vifaa na vipuri, wataalamu wetu wa ndani waliweza kutengeneza sehemu zote zinazohitajika. Kwa bahati nzuri, cyclotron ilianza tena kazi jana na itachangia uzalishaji wa dawa za mionzi,” alisema.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha