5 Januari 2026 - 23:27
Umoja wa Kishia Wakaribia Kufikia Uamuzi wa Mwisho: Nani Atakuwa Waziri Mkuu Ajaye wa Iraq?

Muungano wa Kisiasa wa Mfuko wa Uratibu wa Kishia nchini Iraq uko karibu kufikia uamuzi wa mwisho kuhusu Waziri Mkuu ajaye, huku wagombea waliobaki wakiwa Nouri al-Maliki, Mohammed Shia al-Sudani na Haider al-Abadi, na uamuzi ukitarajiwa kufanyika kwa mujibu wa ratiba ya kikatiba.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Kadri muda wa kikatiba unavyozidi kukaribia nchini Iraq, muungano wa kisiasa wa Mfumo wa Uratibu wa Kishia (Coordination Framework) unaelekea katika hatua ya mwisho ya kufanya uamuzi muhimu utakaobainisha hatima ya serikali ijayo ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za kisiasa, muungano huo unatarajiwa kufanya kikao muhimu jijini Baghdad kwa lengo la kupitia maendeleo ya kisiasa ya hivi karibuni na mchakato wa uteuzi wa Waziri Mkuu ajaye wa Iraq, kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya nchi hiyo.

Vyanzo vya karibu na muungano huo vimeeleza kuwa, licha ya majina tisa kutajwa awali kwa ajili ya wadhifa wa Waziri Mkuu, majadiliano ya kina yamepelekea kupungua kwa wagombea hadi watu watatu pekee, ambao ni:
1_Nouri al-Maliki
2_Mohammed Shia al-Sudani
3_Haider al-Abadi

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Al-Maalouma, majina haya matatu ndiyo yenye nafasi kubwa zaidi ya kupata uungwaji mkono wa muungano wa Kishia.

Ripoti zinaonyesha kuwa kuna ushindani wa kisiasa, usiotangazwa wazi, kati ya Mohammed Shia al-Sudani na Nouri al-Maliki, huku matokeo ya kikao cha sasa yakitarajiwa kuamua iwapo muungano utafikia mgombea mmoja wa pamoja, au kuchelewesha uteuzi huo hadi baada ya kuchaguliwa Rais wa Iraq na vyama vya Kikurdi.

Katika muktadha huo, Abbas Sarout, aliyekuwa mbunge wa Iraq, amesema kuwa mikutano ya hivi karibuni ya viongozi wa Mfuko wa Uratibu wa Kishia imefanikiwa kuleta maelewano kuhusu sifa na vigezo vya mgombea anayefaa kuiongoza serikali ijayo.

Ameongeza kuwa jina la mgombea wa muungano huo litatangazwa mara tu mchakato wa uchaguzi wa Rais utakapokamilika, kwa mujibu wa ratiba ya kikatiba, akisisitiza kuwa muungano huo kama kundi kubwa bungeni hautachelewesha mchakato huo.

Sarout amesisitiza kuwa tofauti za maoni ndani ya muungano hazimaanishi mgawanyiko au mgogoro wa kisiasa, bali ni mitazamo tofauti itakayopata suluhu katika muda mfupi ujao.

Kwa upande wake, Zuhair al-Jalabi, mwanachama wa muungano wa Dawlat al-Qanun, amesema kuwa hakuna mkwamo wa kisiasa katika mchakato wa uteuzi wa Waziri Mkuu, na kwamba suala hilo litakamilika kwa wakati uliopangwa kikatiba.

Aidha, Abu Mithaq al-Massari, mwanachama wa ofisi ya kisiasa ya Shirika la Badr, amesema kuwa hadi sasa muungano huo umezingatia majina matatu tu - Al-Maliki, Al-Sudani na Al-Abadi - na kwamba hakuna mgombea wa nne anayezingatiwa rasmi.

Ameongeza kuwa baadhi ya tetesi zinazotolewa na vyombo vya habari hazilingani na uhalisia wa majadiliano yanayoendelea ndani ya muungano huo.

Kwa jumla, Mfuko wa Uratibu wa Kishia umeweka mkazo mkubwa juu ya kuheshimu muda wa kikatiba na kuunda serikali mpya ya Iraq kwa wakati uliopangwa, huku ukisisitiza kuwa makubaliano ya mwisho yako karibu kufikiwa.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha