Profesa Saeed Adeq wa sosiolojia ya siasa katika Chuo kikuu cha Marekani mjini Cairo anasema, ingawa hali inaonekana kuwa shwari, lakini kihalisi hali si shwari. Ametolea mfano maandamano makubwa nchini Misri, mvutano wa kisiasa uliosababisha mgawanyiko kati wa wananchi, na pia kushuka kwa uchumi. Ameonya kuwa mwaka huu utakuwa wa machafuko makubwa nchini humo.
Jumamosi iliyopita, chama kikuu cha upinzani nchini Misri, National Salvation Front, ambacho awali kilikubali kushiriki kwenye mjadala wa kitaifa ulioandaliwa na rais Mohamed Morsi wa Misri, kimesema kinakubaliana na matakwa ya wananchi ya kuondoa utawala uliopo madarakani sasa na udhibiti wa chama cha Muslim Brotherhood. Chama hicho pia kimesema hakitashiriki majadiliano hayo mpaka pale umwagaji damu nchini humo utasimamishwa na kuchunguzwa. Madai hayo yanatokana na picha ya video inayowaonyesha askari wa ulinzi wakimpiga vibaya mtu mmoja kwa virungu, na kwamba rais Morsi ametoa amri ya kutumia njia zozote ili kusitisha maandamano.
Wachunguzi wanaamini kuwa, kujiondoa kwa NSF katika mjadala wa kitaifa kuna athari mbaya kwa chama hicho. Ahmad Qandil, mtaalam wa masuala ya siasa katika Chuo cha elimu ya maarifa ya siasa cha Ahram nchini Misri anasema, utafiti uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya wamisri hawajafurahia kitendo cha NSF. Amesema hivi sasa Wamisri hawaamini tena siasa kwa ujumla, na kinachotakiwa sasa ni kwa serikali na upande wa upinzani kuchukua njia ya mazungumzo ili kusuluhisha masuala ambayo bado hayajapata ufumbuzi na kurejesha imani kwa wananchi. Baadhi ya waandamanaji jana walijaribu kuvamia vituo vya polisi vya mjini Tana, jimboni Gharbiya, kilomita 80 kutoka mji mkuu wa Misri, Cairo, kufuatia kuuawa kwa mwanaharakati wa kisiasa.
Qandil amesema, utulivu ulioko sasa nchini Misri hautadumu kwa muda mrefu, na kwamba kila kitu kinategemea utayari wa vyama vya kisiasa vinavyopingana kufanya mazungumzo ya kweli na kufikia makubaliano. Bila ya hivyo, umwagaji damu utashuhudiwa tena nchini Misri.