30 Mei 2020 - 07:01
Kuongezeka maonyo dhidi ya Israel kuhusu kuunganishwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan

Katika hali ambayo Benjamini Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel tayari ameainisha taraehe ya kuunganisha Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo (Israel), maonyo yanaendelea kutolewa dhidi ya hatua hiyo hatari.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Bejamini Netanyahu kiongozi wa chama cha Likud na Benney Gantz, kiongozi wa chama cha Buluu na Nyeupe, baada ya kuafikiana kubuni serikali ya pamoja kwa lengo la kuhitimisha mkwamo wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya siku 500 katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, walitangaza kwamba wataunganisha sehemu ya ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na  ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo. Netanyahu na waziri wake wa mambo ya nje, Gabi Ashkenazi, hivi karibuni pia walitangaza kuwa watatekeleza mpango wa kuunganisha sehemu ya ardhi za Ukingo wa Magharibi na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu kuanzia mwanzoni mwa mwezi ujao wa Juni.

Sisitizo la kuunganishwa ardhi hizo na zile zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Tel Aviv kwa hakika linatokana na masuala mawili muhimu. La kwanza ni uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani kwa utawala huo ghasibu na la pili ni ushirikiano wa baadhi ya nchi vibaraka za Kiarabu katika uwanja huo. Bila shaka uunganishwaji huo wa Ukingo wa Magharibi ni msingi muhimu katika mpango wa ubaguzi wa rangi wa 'Muamala wa Karne' uliozinduliwa na Rais Donald Trump wa Marekani mnamo tarehe 28 Januari mwaka huu. Ni jambo lisilo na shaka kwamba Israel imechukua uamuzi wa kuziunganisha ardhi hizo za Ukingo wa Magharibi na ardhi zingine za Wapalestina unazizokalia kwa mabavu kutokana na uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani.

Katika uapande wa pili, utawala huo wa Kizayuni umepata kiburi cha kutekeleza mpango wake huo wa kibaguzi kutokana na kimya na hata ushirikiano wa baadhi ya nchi vibaraka za Kiarabu. Ushirikiano huo ni mkubwa kiasi kwamba hata baadhi ya vyanzo vya Kizayuni vinasema kuwa tishio la hivi karibuni la Jordan dhidi ya kuunganishwa sehemu ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan halina umuhimu wowote. Kuhusu suala hilo, gazeti la Israel la Yahom limeandika kuwa: 'Mfalme Abdalla wa Pili wa Jordan katika hotuba yake kwa watu wa nchi hiyo alizungumzia mambo mengi kuhusu kuasisiwa kwa nchi hiyo hadi mafanikio yake ya karibuni katika kupambana na virusi vya corona, lakini nukta ambayo hakuigusia katika hotuba hiyo hata kwa neno moja tu ni kuhusu msimamo rasmi wa nchi hiyo kuhusu suala la kuunganishwa Bonde la Jordan na vilevile baadhi ya sehemu za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.' Gazeti hilo la Kizayuni linaendelea kuandika: 'Katika mahojiano yake na jarida la Ujerumani la Der Spiegel, Mfalme Abdalla wa Pili alijiepusha hata kuashiria nukta hii kwamba huenda uunganishwaji huo ukapelekea kufutiliwa mbali mapatano ya amani na Israel.'

Pamoja na hayo ni wazi kwamba sisitizo la utawala haramu wa Israel la kutekeleza mpango wake wa kuunganisha sehemu ya ardhi za Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na ardhi unazozikalia kwa mabavu litakuwa na matokeo mengi makubwa. Moja ya matokeo hayo ni kufutiliwa mbali mapatano ya amani kati ya utawala huo ghasibu na Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Inasemekana kuwa Mohammed Ashtieh, Waziri Mkuu wa Palestina tayari ameshatangaza msimamo huo na pia utawala haramu wa Israel umefahamishwa jambo hilo. Akizungumza katika kikao na mabalozi wa nchi kadhaa za Kiarabu, Mohammed Ashtieh Amesema kuwa kufuatia matamshi ya hivi karibuni ya Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuwa malaka hiyo itafutilia mbali mikataba yote iliyotiliana saini na utawala huo wa kibaguzi, mamlaka hiyo tayari imesimamisha ushirikiano wake na utawala huo katika nyanja zote.