Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Indhari za mashirika hayo zimetolewa ikiwa imeshapita takriban miaka sita tangu vilipozuka vita ambavyo vimeifanya asilimia 80 ya raia wa nchi hiyo iishi kwa kutegemea misaada ya kibinadamu.
Kwa mujibu wa ripoti ya pamoja iliyotolewa jana Ijumaa na mashirika manne ya Umoja wa Mataifa ya Mpango wa Chakula WFP, Shirika la Chakula na Kilimo FAO, Shirika la Kuhudumia Watoto UNICEF na Shirika la Afya Duniani WHO, katika mwaka huu wa 2021 kutakuwa na ongezeko la asilimia 22 la watoto wa umri chini ya miaka mitano watakaokabiliwa na hali mbaya sana ya lisheduni.
Hali mbaya kupindukia ya lisheduni inamaanisha mtu kukabiliwa na hatari ya kifo cha kukosa chakula.
Mkurgenzi Mtendaji wa WFP David Beasley ameeleza katika ripoti hiyo ya pamoja kwamba Aden, Hudaydah, Taiz na mji mkuu wa Yemen Sana'a ni miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa vibaya zaidi na baa hilo la njaa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto wengine milioni mbili na laki tatu wenye umri chini ya miaka mitano wanahofiwa kukumbwa na hali mbaya kupindukia ya lisheduni katika mwaka huu wa 2021.
Aidha akina mama wajawazito au wanaonyonyesha milioni moja na laki mbili nao pia wanahofiwa kukumbwa na hali hiyo katika kipindi cha mwaka huu.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, kwa sasa, Yemen ndio nchi inayokabiliwa na hali mbaya zaidi ya kibinadamu duniani.
Ikumbukwe kuwa, msaada na uungaji mkono wa Marekani, Imarati na nchi zingine kadhaa, mwezi Machi 2015 Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa nchi kavu, baharini na angani. Moto wa vita uliowashwa na Saudia na washirika wake, hadi sasa umeshateketeza roho za watu zaidi ya 16,000 nchini Yemen, mbali na kujeruhi makumi ya maelfu pamoja na kusababisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.
Aidha mzingiro huo ambao muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia umeiwekea Yemen, umeisababishia nchi hiyo masikini ya Kiarabu uhaba mkubwa wa bidhaa za mahitaji ya lazima zikiwemo za chakula na dawa.../
342/