Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Majalis za Muharram katika kuomboleza shahada ya Imam Hussein (as) zinaendelea kila siku katika Mwezi huu Mtukufu wa Muharram. Darsa mbalimbali zinaendelea kutolewa zikiwa zimesheheni mafunzo mbalimbali ya Kiislamu yanayopatikana katika Harakati ya Mapinduzi ya Mapinduzi ya Imam Hussein (as). Leo hii imewasilishwa mada muhimu kuhusiana na "Tofauti kati ya Mtu anayemjua Imam Hussein (AS) na Asiyemjua". Mwasilishaji wa mada hii ni Samahat Sheikh Sheikh Abdul Rahman Kachere. Zifuatazo ni nukta muhimu zilizokuja katika khutba yake:
1- Mtu Anayemfahamu Imam Hussein (AS) Daima ni Jasiri Katika Kukabiliana na Dhulma
Mfano: Yanayotokea Mashariki ya Kati, watu wanaopinga dhulma ni wale wanaomfahamu na kumuelewa Imam Hussein (AS).
2- Wale wasiomjua Imam Hussein (AS) ni rahisi kunyonywa rasimali zao, kutumika vibaya na kudanganyika
Kwa mfano: Tizama ni nini kinatokea katika (baadhi ya) nchi za Kisunni zinazoongozwa na serikali za kifalme!, Utaona zinashirikiana na Marekani na Magharibi dhidi ya Waislamu wengine wa Madhehebu ya Shia na hata wa Madhehebu ya Sunni (Kama vile waislamu wa Palestina, wanaouliwa kila siku na serikali hizo za kifalme zinaendelea kuunga mkono utawala wa Israel unaoua waislamu wa Palestina ambao kimadhehebu ni Masunni wenzao, lakini wao wanasapoti Marekani na nchi za Ulaya na kufanya kile wanachokiita: "Uhusiano wao wa Kawaida na Israel").
Pia katika nchi za Kiafrika. Migogoro ya kikabila Barani Afrika na vita kati ya makabila, kama vile vinavyoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda, siri ya migogoro hiyo yote ni kutomjua vizuri Imam Hussein (as) na hatimaye kutumbukia katika michezo ya Marekani na Wamagharibi ambao daima wanafaidika na machafuko yoyote yanayoendelea kokote duniani - hususan katika nchi hizo za Bara la Afrika.
Kumjua vizuri Imam Hussein (as) na mapambano yake dhidi ya dhulma na udhalimu, kutawafanya watu wa mataifa mbalimbali kumpinga adui na dhalimu, na kutambua njama za adui na dhalimu dhidi ya mataifa yao, na kuwa tayari kupambana kwa ajili ya kuinusuru Haki, kwa ajili ya kuondoa uistikbari, dhulma na unyonyaji wa mfumo mpya wa ukoloni unaoitwa: Ukoloni mambo leo.
Your Comment