Main Title

source : Parstoday
Ijumaa

2 Septemba 2022

15:52:46
1302713

UN yawahamishia Rwanda watafuta hifadhi 100 kutoka Libya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limetangaza kuwa limewahamishia nchini Rwanda makumi ya watu wanaotafuta hifadhi waliokuwa nchini Libya.

Taarifa ya UNHCR imesema, miongoni mwa watu hao 100 wanaotafuta hifadhi na waliohamishiwa nchini Rwanda ni watoto 38 kutoka nchi tofauti za Afrika.

Kadhalika shirika hilo la Umoja wa Mataifa limezishukuru mamlaka za Libya kwa kufanikisha mpango huo wa kuwahamishia nchini Rwanda wahajiri wa Kiafrika.

Katika hatua nyingine, shirika la kutetea haki za binadamu la Medical Justice limeikosoa vikali serikali ya Uingereza, kwa kutaka kuwahamishia nchini Rwanda watafuta hifadhi walioko katika nchi hiyo ya Ulaya.

Ripoti ya shirika hilo imefichua kuwa, baadhi ya wahajiri hao wanaotazamiwa kupelekewa Rwanda ni wahanga wa mateso, unyanyasaji na magendo ya binadamu.

Medical Justice imebainisha kuwa, baadhi ya wahajiri iliyowahoji wakiwemo wanawake na watoto wadogo wana historia ya matatizo ya kisaikolojia, hivyo kuwapeleka Rwanda ni kuwaongezea matatizo.

Uamuzi wa serikali ya Uingereza wa kuwahamishia Rwanda watafuta hifadhi wanaokwenda nchini humo chini ya makubaliano tata na Kigali umeendelea kukosolewa ndani na nje ya nchi mbili hizo.

342/