Hayo yameelezwa na Dkt. Philip Mpango, Makamuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika hotuba yake kwenye mkutano wa 77 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kuongeza kuwa, sambamba na hilo, “suala la Afrika kuwa limeenguliwa kwenye upataji wa chanjo, lilipatia msisitizo umuhimu nchi za Afrika kushirikiana kuzalisha na kukuza majawabu ya kiasili kupitia tafiti za pamoja na kisayansi na kitabibu.”
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameeleza kuwa, janga la corona limeibua umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye elimu ya afya ya umma, hususan elimu ya kinga kwa kujenga uwezo wa mwili wa mtu kujikinga kwa kufanya mazoezi ya mwili, lishe bora na mifumo ya maisha.
Ameongeza kuwa, ingawa usaidizi wa kimataifa kwa Afrika katika kukabili kusambaa kwa COVID-19 kwa kupatia vifaa vya uchunguzi, dawa, fedha na chanjo ulichelewa, lakini ulikuwa muhimu katika kushinda vita dhidi ya janga hilo.
Dkt. Philip Mpango amesema katika sehemu nyingine ya hotuba yake kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa mataifa kwamba, kwa sasa Tanzania inaendelea na kampeni ya chanjo na hadi tarehe 11 mwezi huu wa Septemba asilimia 60.56 ya watu wanaopaswa kupatiwa chanjo dhidi ya COVID-19 walishachanjwa.
Makamu wa Rais wa Tanzania amegusia pia suala linalotakiwa hivi sasa la nchi kuhama kutoka nishati kisukuku na kuelekea katika nishati salama akisema serikali yake inapongeza hatua zote zinazochukuliwa kudhibiti uharibifu wa mazingira.
342/