Main Title

source : Parstoday
Jumapili

4 Juni 2023

09:34:09
1371065

Kasisi wa Kiafrika: Imam Khomeini (RA) alikuwa kiongozi mwenye nguvu na fikra ya kimataifa

Kasisi wa Afrika Kusini ametangaza kwamba fikra za mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ayatullah Ruhullah Khomeini zilikuwa na taathira kubwa kwa watu na siasa nchini Iran na meneo menginezo ya dunia.

Kasisi Allan Boesak ameyasema hayo kwa mnasaba wa siku ya leo (Juni 4, 2023) ya kumbukumbu ya kifo cha Imam Khomeini (RA), mwanzilishi mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Allan Aubrey Boesak kasisi wa Kanisa la Kiholanzi la Afrika Kusini na mwanasiasa na mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi huko Cape Town, Afrika Kusini, amesema katika mahojiano na mwandishi wa Iranpress kwamba Imam Khomeini alikuwa kiongozi mwenye imani madhubuti na aliamini na kutenda kila alichosema. 

Kasisi huyu wa Kiafrika amesisitiza kwamba nguvu na fikra za Imam Khomeini ziliwaathiri watu kutoka Ufaransa hadi Iran na kuwafanya watu waamini uwezo wao.

Mchungaji Alan Boesak ameongeza kuwa, mafanikio makubwa zaidi ya Imam Ruhullah Khomeini ni kuwawezesha na kuwaamsha wananchi ili kufanya mabadiliko katika jamii ya Iran.

Mwanaharakati huyo wa kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini amesema kuwa Imam Khomeini alijua kwamba siasa hazitakuwa na maana yoyote kiutendaji iwapo hazitaunganishwa na imani za kidini na maadili, na kwamba siasa inapaswa kuwasaidia watu kupinga dhulma.

Alan Boesak amesisitiza kuwa, uamuzi wa Imam Khomeini wa kuvunja uhusiano wa Iran na Israel na kupinga utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini (baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu) ulikuwa hatua muhimu sana na kubwa ambayo hakuna nchi yoyote katika eneo la Mashariki ya Kati iliyowahi kuchukua.

Kasisi huyo wa Kiafrika amesema kuwa baada ya matukio ya mwaka 1979, nchi za Magharibi zilianzisha vikwazo na mashinikizo dhidi ya Iran na kuzidisha vikwazo hivyo mwaka baada ya mwingine ili kuilazimisha Iran isalimu amri, lakini Jamhuri ya Kiislamu ilisimama kidete, na msimamo huo umekuwa na taaathira katika milingano ya kimataifa.

342/