Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Rais wa Shirika la Waqfu na Misaada ya Kidini nchini Iran, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sayyid Mahdi Khamoushi, amesema kuwa matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein (a.s) si tukio la kawaida, bali ni harakati ya kuunda ustaarabu mpya na inayobeba maana ya kujitolea, mashahidi na kusimama imara dhidi ya dhulma na ubeberu.
Akizungumza katika kongamano maalum la “Hatua za Kimbinguni” lililowaleta pamoja waandaaji wa mahema ya Arubaini huko kwenye Haram ya Sheikh Sadouq (r.a), alisisitiza kuwa harakati hii ni kielelezo cha mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya mabeberu na inapaswa kuwa sauti ya Umoja wa Kiislamu Duniani.
Ameongeza kuwa:
“Arubaini ni taswira ya utamaduni wa kustahmili kuongojea (Kudhihiri kwa Imam wa Zama) na kujitolea. Hii si tu ibada ya kutembea, bali ni safari ya kujifunza maana halisi ya kuwa huru, kuongojea (Kudhihiri kwa Imam wa Zama) na Kufa Kishahidi. Kwa anayetamani kuelewa maana ya kweli ya 'intidhar', basi ajitose katika harakati ya Arubaini."
Kwa mujibu wa riwaya mbalimbali alizozitaja, amesisitiza kuwa kutembea kuelekea Karbala kwa kumtambua Imam Hussein (a.s) kwa haki yake, kunaleta malipo makubwa ya kiroho ikiwa ni pamoja na msamaha wa madhambi yote na ujira wa Hijja na Umra nyingi zilizokubaliwa.
Akiashiria hotuba ya 168 ya Nahjul Balagha kuhusu uhusiano wa watu na watawala, amesema kuwa:
“Mapambano ya Jihadi ya Imam Hussein (a.s) yalikuwa ni kudhihirisha uhusiano huo kwa njia ya kipekee, na adui anapotaka kuvunja Umoja wa Waislamu hushindwa kwa sababu ya uongozi wa kidini na ufuasi wa Waislamu kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi.”
Hujjatul-Islam Khamoushi amesisitiza kuwa msafara wa Arubaini ni fursa ya kumwambia Imam wa Haki:
"Tuko nyuma yako", na kusimama na uongozi wa kidini unaopambana na Ubeberu na Uistikbari wa Kimataifa.
Amesema kuwa:
“Leo, Iran iko kileleni katika kupinga ubeberu na uistikbari, na sauti ya mapambano yake inasikika duniani kote. Tunapaswa kuonyesha kuwa tupo nyuma ya Kiongozi wetu wa Mapinduzi wa Kiislamu, tukimfuata kwa dhati. Kama alivyosema Imam Khomeini (r.a):
‘Hatuna tatizo na Dunia, isipokuwa na utawala wa kibaguzi na wa Kizayuni’.”
Akamaliza kwa kusisitiza kuwa:
“Arubaini ya mwaka huu inapaswa kuleta tumaini kwa Waislamu na kuwavunja nguvu maadui. Umoja ndiyo njia ya wokovu kwa Ulimwengu wa Kiislamu na Bendera ya Mapambano dhidi ya mfumo wa kishetani lazima ibaki juu.”
Your Comment