Main Title

source : Parstoday
Alhamisi

12 Septemba 2024

12:41:57
1484686

Iran yaazimia kuimarisha uhusiano na Burkina Faso

Balozi wa Iran nchini Burkina Faso, Mojtaba Faqihi amekutana na Abubakar Nakanabo, Waziri wa Uchumi na Fedha wa taifa hilo la Afrika Magharibi na kujadili umuhimu wa kupanua ushirikiano wa pande mbili katika nyuga za kiuchumi, kiufundi na kibiashara.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Faqihi na Nakanabo jana Jumatano walijadili nafasi na jukumu la Wizara ya Uchumi na Fedha ya Burkina Faso la kuunga mkono na katika hali muhimu kutoa dhamana ya serikali kutekeleza miradi ya viwanda na miamala baina ya nchi hizo mbili.

Pande hizo mbili zimetia saini hati 9 za ushirikiano, na kujenga misingi faafu kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili, zikiwa na kamisheni ya kwanza ya pamoja ya ushirikiano wa kiuchumi, kiviwanda na kiutamaduni kati ya Iran na Burkina Faso miaka miwili iliyopita.

Makampuni ya serikali na wafanyabiashara wa sekta binafsi kutoka Iran na Burkina Faso wamefikia maelewano mazuri, ambayo iwapo vikwazo vya kibenki vitatatuliwa, vitashuhudia ongezeko kubwa la mauzo ya bidhaa na huduma za kiufundi na kihandisi za Iran katika nchi hiyo ya Kiafrika.

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amekuwa akisisitiza kuwa, sera za Jamhuri ya Kiislamu ni kushirikiana na kupanua uhusiano na nchi zote za dunia zikiwemo za Afrika.

Hivi karibuni pia, Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi alisema kuwa kipaumbele cha kwanza katika sera za kigeni ni nchi jirani na kipaumbele cha pili ni kupanua uhusiano na Afrika na Asia Mashariki.

342/