Wanasema kuwa, hatua hiyo itasaidia kupunguza ndoa za utotoni huku wakisema uwepo wa sheria hiyo umekuwa kichochezi kikuu cha ndoa za utotoni kutokana na baadhi ya wazazi kutumia sheria hiyo kukandamiza haki za watoto wao.
Tafiti zilizofanywa na taasisi ya Msichana Initiative nchini Tanzania zimebainisha kuwa, katika kila matukio 10 yaliyoripotiwa ya vitendo vya ukatili matukio nane yamebainika kuhusisha watoto wa kike suala linaloashiria kuwa watoto hao ni waathirika wakubwa wa vitendo vya ukatili.
Tafiti hiyo imebainisha watoto wa kike kuendelea kukabiliana na vitendo vya ukatili mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia, ukatili wa kisaikolojia, kukosekana kwa fursa sawa za elimu, mimba za utotoni pamoja na ndoa za utotoni kama anavyoeleza Fundikila Wazambi Mtafiki kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC).
Tafiti hiyo imeendelea kubainisha kuwa, idadi kubwa ya watoto wa kike wanaoishi maeneo ya vijijini wameendelea kukumbana na changamoto ya ndoa za utotoni kutokana na sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kutoa ruhusa kwa mtoto wa kike kuolewa akiwa na umri wa miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi au mahakama.
parstoday