Main Title

source : abna.ir
Jumamosi

18 Oktoba 2014

14:48:43
645190

Sehemu ya kwanza

Je Kuna umuhimu wa kuwepo Dini?

Kusema kweli, hakuna serikali itakayomzuia mtu huyu asiibe lakini Dini inaweza,

DINI NI NINI?
Dini ni neno lenye asili ya lugha ya kiarabu na linatumika katika maana zifuatazo:
(1) Dini inamaana ya "Desturi;Sheria; Tabia;Mazoea.
(2) "Hukumu; Thawabu au Adhabu; Hesabu Amri; Sheira."
Maana hizi, nazo pia, zahusiana zenyewe kwa zenyewe na zatushabihisha kwenye imani ya Maisha ya Akhera.
Zingatia:Maana hasa ya neno hili Diin ni kuwa mwanadamu kwa silika zake za asili, hana budi kuwa na mpango wa maisha wenye msingi wa fikra za kiroho au fikra zile tuziitazo "Imani".
Hivyo basi, inaonekana kuwa, neno "Din" lina maana kubwa mno kuliko ile ya neno la Kiingereza "Religion", ambayo husisitiza maana ya Mwanadamu kuitambua Nguvu kubwa kuliko yeye, na ambayo inautawala ulimwengu mzima, na hasa Mungu au miungu ya mtu kibinafsi, ipasikayo kutiiwa na kuabudiwa; matokeo ya utambuzi wa aina hiyo; mwongozo wa kiroho wa mtu; au mpango maalum wa Kiimani na kiibada.

FAIDA ZA DINI NI ZIPI
Zipo sababu nyingi zimfanyazo mwanadamu ahitaji Dini.
(1) Sote twajua kuwa mwanadamu ni mnyama ahitajiye kuishi kijamii pamoja na wenzake. Kila mtu anategemea mamilioni ya watu wenzake kwa maisha yake na kwa mahitaji muhimu ya hayo maisha yake. Pia tunajua kuwa kila jamii inahitaji sheria fulani fulani ili kuzuia dhulma na kuhifadhi haki ya kila mtu katika jamii hiyo.
Kama ni hivyo, Je,ni nani aliye na haki ya kutunga Sheria hizo?
Je Itungwe na mtu mmoja? (mtu huyo na awe mfalme au mtawala,mzimu)!
Jibu ni "Hapana." Mtu mmoja hataweza, maana kwa mujibu silika na tabia za kibinadamu, atatunga sheria kwa kufuatana na tamaa na maslahi yake ya kibinafsi.
Je Itungwe kikundi cha watu? (Watu hao na wawe wa kikundi cha Utawala wa watu wa koo Bora au wa kikundi cha kidemokrasi,wabunge, wazee wa hekima, wanafalsafa na nk)! Jibu ni kuwa,?
Jibu kitakuwa "Hawa pia hawataweza kuifanya kazi hiyo vipasikavyo, maana kila mmoja wao hawezi kujiepusha na uamuzi usio sawa na wingi wa uamuzi usio, sawa, hauwezi kupatana na uamuzi ulio sawa.
(2) Vile vile ni dhahiri kuwa hakuna kikundi cha watu kiwezacho kujiepusha na kujitia katika tamaa za kibinafsi. Kwa mfano katika siku za utawala wa kikoloni, mabunge na halmashauri za Makoloni zilikuwa zikitunga sheria kufuatana na mapendekezo ya watawala wa Kizungu. Siku hizi, mabunge na Halmashauri hizo hizo hutunga sheria kufuatana na mapendekezo ya wananchi. Kujali ubinafsi kulikuwa na bado kungali katika utungaji wa sheria duniani kote.
(3) Zaidi ya hapo hakuna mtu au kikundi cha watu chenye uwezo wa kutunga sheria za mambo mengi na ambazo zimo katika msingi wa usawa na uadilifu kamili.
Zingatia:Kwa sababu hiyo, ni lazima sheria hizo zitungwe na mjuzi ambaye ni mbora kuliko mwanadamu, ambae hana chochote cha kupoteza au cha kufaidika nacho kutokana na sheria hizo, na ambae kila mwanadamu ana uhusiano wa aina iliyo sawa kwake. Kwa lugha rahisi Mjuzi huyu asiwe na maslahi binafsi katika kutunga sheria hiyo.
Na bila shaka mtaalamu huyo atakuwa ni MWENYEZI MUNGU pekee,Kwa sababu hiyo tunawajibikiwa kuwa na dini.
(4) Zaidi ya hapo ni kuwa, sheria na desturi zilizotungwa na mwanadamu zina upungufu mmoja mbaya sana: Sheria na desturi hizo haziwezi kuzuia matendo ya jinai hasa za siri. Upungufu huu,umesababisha sheria za namna hii kuonekana hazina faida za kudumu.
Kwa mfano, Muhalifu anaingia nyumba isio na watu, katika kijiji cha ughaibuni, usiku wa manane kwa ajili ya kuiba na kupora vitu vyenye thamani. Muhalifu huyu anaelewa bayana kuwa hakuna mtu aiwakilishaye Serikali, hakuna mlinzi wala polisi katika sehemu hiyo. Hivyo muhalifu huyu hufanya jinai zake kwa utulivu na amani kwani anahisi hakuna sheria ya kumkamata.
Swali la kujiuliza ni kwamba Je! Katika hali kama hii, kuna sheria ya serikali ambayo itamzuia muhalifu huyu kutimiza jinai hii?
Bila shaka jibu litakuwa ni "HAPANA".
Kusema kweli, hakuna serikali itakayomzuia mtu huyu asiibe lakini Dini inaweza, Dini iliyo ya kweli, kama tulivyoieleza hapo juu, huwafundisha watu kuwa yupo Mwenyezi Mungu, ambae ajua kila kitu na anayeona kila kitu, anaona vya wazi na vilivyofichika. Mwenyewe ni Mwadilifu na Mwema na anatutaka nasi tuwe waadilifu na wema; na kwamba kila kitu tunachokifanya tutakuta malipo yake siku maalumu baada ya kufa kwetu.
Kama mtu atakuwa na imani ya Dini kama inavyotakiwa,anaweza kujiepusha na kutenda jinai,ufuska, dhulma,ufisadi na dhambi ya aina yeyote popote atakapokuwa.
Sheria za serikali zinaweza kuzuia mtu kutenda matendo mabaya ya wazi wazi na hata hivyo, ni katika muda na mahali ambapo mikono ya serikali hiyo yaweza kufika. Lakini kumwamini Mwenyezi Mungu na kuwa na imani ya dini,situ kwamba humzuia mtu kufanya jinai za wazi na kificho bali humzuia hata kufikira kufanya jinai na madhambi.
Utawala huu, hauna mipaka ya muda wala sehemu,kwa sababu Mwenyezi Mungu yupo kila mahali na anaona kila kitu.
(5) Ili kuzielewa vizuri faida zilizo wazi wazi, ambazo jamii yazipata kutokana na imani ya kuwepo Mwenyezi Mungu na dini, hebu jaribu kufikiria machafuko na ghasia ambazo wanaadamu wangeliweza kujitia, kama imani ya kuwepo Mungu ingalitupiliwa mbali.
Hakutakuwa na jamii yoyote yenye heshima na taadhima, badala yake, kutakuwa na umati na makundi watu wasio na mpangilio.
Katika hali hiyo, kila mmoja atakuwa uhuru wa kufanya chochote kile akipendacho, kuiba,kuchukua mke wa mtu, aslani kutakuwa hakuna mke wamtu, wala mali ya mtu maalum.
Mtu anayefikiria kuwa hakuna Mungu, na hakuna maisha baada ya kifo, na kuwa yeye amekuwepo hapa duniani kwa sudfa na bahati tu bila ya hekima wala malengo. Mtu huyu atahisi kuwa muda wa maisha ni mfupi. Kwa hivyo, kwa kawaida atashawishika na kuyafaidi maisha kwa kadri iwezekanavyo bila ya kujali kitu chochote kile.
Kitu atakacho kiwaza ni kujaribu kuepekana na kukamatwa akiwa anatenda jambo lolote baya, au kuonwa na serikali tu au jambo litakalo mletea madhara ya kudhuru uhai wake. Kinyume na hapo muda wote atajiona kuwa yu salama, na hataacha kutenda jinai lolote ili kujikidhia tamaa zake, bila ya kujali dhara la tamaa yake hiyo kwa wenzake.
Yamkini ukaliza kwamba: Hata Mpagani (mtu asiyeamini kuwa kuna Mungu) anaweza kuishi maisha mema kama yale ya mfuasi wa dini. Kama jambo hili lawezekana bila ya dini, nini basi faida ya dini?
Nitakujibu: Ni kosa kufikiria kuwa, maisha mema ya Mpagani hayana uhusiano kabisa na dini; kwa sababu fikra hizo njema hazikuhifadhiwa akilini mwa mtu huyo na kitu kingine chochote ila na dini tu. Kwani mafundisho mema ya kidini yameimarishwa akilini mwa mwanadamu kwa maelfu ya miaka. Yamekuwa yakihifadhiwa toka na kuhama toka kizazi mpaka kizazi, kwa njia ya asili ya mwanadamu ya mwana kurithi tabia za wazazi, marafiki, jamii na mazingira yanayomzunguka. Hii ndio sababu ya mpagani huyu kuwa na asili ya matendo mema yanayokubalika kiakili.
Katika mada ijayo Mungu akiniwezesha nitajaribu kuelezea fikra na sababu zilizopelekea baadhi ya watu kupinga dini.