Main Title

source : Pars Today
Alhamisi

30 Mei 2019

08:23:50
945437

Muamala wa Karne; muamala muovu na jinai dhidi ya haki za taifa la Palestina

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa "Muamala wa Karne" uliopendekezwa na Marekani kuhusu Palestina ni muamala muovu sana na kwamba kikao kilichopangwa kufanyika mwezi ujao huko Bahrain kujadili mpango huo nacho kitatumbukia kwenye moto wa jahannam kama ilivyo kwa muamala huo wa karne.

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa "Muamala wa Karne" uliopendekezwa na Marekani kuhusu Palestina ni muamala muovu sana na kwamba kikao kilichopangwa kufanyika mwezi ujao huko Bahrain kujadili mpango huo nacho kitatumbukia kwenye moto wa jahannam kama ilivyo kwa muamala huo wa karne.

Mahmoud Abbas alisema hayo Jumatatu usiku na kusisitiza kuwa mpango wa Muamala wa Karne hauwezi kutekelezwa kwani utatuzi wa kadhia ya Palestina ni njia ya kisiasa tu. 

Kikao cha Bahrain ambacho kimetajwa kuwa ni hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mpango wa "Muamala wa Karne" kinatarajiwa kufanyika tarehe 25 na 26 mwezi ujao wa Juni 2019 mjini Manama. Kikao hicho kimeitishwa kwa uungaji mkono wa baadhi ya tawala za kiimla za Kiarabu na moja ya malengo yake ni kuhakikisha nchi za Kiarabu zinakuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao mikono yake imejaa damu za watu wasio na hatia hasa Wapalestina.

Rais wa Marekani, Donald Trump alipendekeza kwa mara ya kwanza mpango wa "Muamala wa Karne" mwaka 2017 na kuzishinikiza tawala za kifalme za Saudi Arabia, Bahrain na Imarati kugharamia fedha za mpango huo. 

Salman Radhawi ni mtaalamu wa masuala ya Palestina ambaye anasema kuhusu muamala wa karne wa Marekani kwamba: Baadhi ya nchi za Kiarabu ndizo zitakazotoa fedha za kuendeshea mpango huo kwa maana ya kwamba Marekani itatoa asilimia 20, nchi zote za Ulaya zitatoa asilimia 10 na Waarabu watatoa asilimia 70 ya fedha za kuendeshea mpango huo

Kwa kuzingatia mgao huo tutaona kuwa lengo la Marekani ni kuendesha mpango wake huo wa karne kwa fedha za mafuta za Waarabu licha ya kwamba hauna mfungamano wowote na uhakika wa kihistoria wa kadhia ya Palestina. Ahadi za Marekani za kulinda usalama wa baadhi ya nchi za Kiarabu ukiwemo utawala wa kiimla wa Saudi Arabia umezisukuma nchi hiyo kwenye kutenda jinai dhidi ya haki ya taifa madhlumu la Palestina.

Jumatatu usiku, Sheikh Issa Qassim, mwanachuoni mwanamapambano wa Bahrain alitoa tamko akisema: Lengo la mpango wa "Muamala wa Karne" ni kutekeleza njama ya pamoja ya Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu dhidi ya kadhia ya Palestina.

Ukweli wa mambo ni kuwa, mpango wa muamala wa karne unakanyaga misingi ya awali kabisa ya malengo matukufu ya Palestina na umejikita zaidi katika masuala ya kipropaganda. Mipango ya huko nyuma ya Marekani kuhusu Palestina nayo yote imefeli. Mazungumzo ya maelewano baina ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Israel ni mfano wa wazi wa mipango iliyofeli huko nyuma ya Marekani. Sababu ya kufeli mipango hiyo yote ni kutokana na kutojali kwake haki za taifa la Palestina.

Kwa upande wake, Hossein Ajourlou, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati anasema: Mipango ya Marekani kuhusu Palestina si tu hadi hivi sasa imeshindwa kutekelezwa lakini pia mipango hiyo yote haina itibari yoyote. Lakini kwa vile Marekani inajiona ndilo dola pekee lenye nguvu duniani linajitokeza kifua mbele kudai kuwa lina mipango ya kutatua kadhia ya Palestina, wakati ukweli wa mambo ni kinyume kabisa na majigambo hayo ya Marekani.

Wataalamu wa mambo wanasema kuwa, mpango wa hivi sasa wa "Muamala wa Karne" hautokuwa na thamani yoyote hasa kwa kuzingatia mshikamano wa wananchi, makundi yote ya Palestina na nchi zote zinazopigania malengo matakatifu wa Palestina katika kuupinga mpango huo. 

Mpango wa Marekani wa "Muamala wa Karne" umedharau haki za mamilioni ya wakimbizi wa Palestina, unahimiza kupokonywa silaha wanamapambano wa Palestina, unataka kuundwe nchi ya Palestina isiyo na jeshi na pia unahimiza kupokonywa Wapalestina na Waislamu mji wao mtakatifu wa Quds na kupewa Wazayuni, yote hayo ni miongoni mwa sababu za kufeli mpango huo wa Marekani hata kabla ya kuanza kutekelezwa. 

Cha kufurahisha zaidi ni kuona kuwa hakuna kundi hata moja la Palestina lililo tayari kushiriki kwenye kikao cha Bahrain na kwamba hatua ya Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kususia kikao cha Bahrain inazidi kuudidimiza chini mpango huo wa Marekani  ulio dhidi ya malengo matukufu ya Palestina.



/129