Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Kwa mujibu wa tovuti ya Sputnik ya Russia, mashambulizi ya anga ya Russia yamekuwa yakiendelea kwa wiki ya tatu mfululizo kwenye ngome za Daesh katika Jangwa la Syria.
Duru za habari katika medani ya vita zimedokezea Sputnik kwamba magaidi wa Daesh hivi sasa wanaendeleza harakati zao katika mkoa wa kaskazini mwa Syria wa Raqqah na mkoa wa kati wa Hama, na ndege za upelelezi zimetambua ngome zao.
Chanzo hicho kimeongeza kuwa, ndege za kivita za Russia zimejibu harakati za magaidi hao kwa kufanya mashambulizi 18, ambapo ngome nne za Daesh ziliharibiwa na magaidi 40 wa wakufurishaji kuuawa na kujeruhiwa.
Aidha duru hizo zimedokeza kuwa wanajeshi vamizi wa Marekani katika eneo la al-Tanf nchini Syria wanatoa msaada mkubwa wa vifaa na kijeshi kwa magaidi wa Daesh, na usaidizi huo unawafikia watu wenye misimamo mikali kupitia barabara za mchanga zinazounganisha majangwa ya Raqqah na Hama.
Mapema mwezi huu, shirika rasmi la habari la Syria SANA, likinukuu vyanzo vya ndani vilivyozungumza kwa sharti la kutotajwa jina, liliripoti kwamba idadi kubwa ya magaidi wa Daesh walikuwa wakipewa mafunzo katika kambi ya Jeshi la Marekani katika mji wa al-Shaddadi wa mkoa wa Hasakah kaskazini mashariki mwa Syria katika siku chache zilizopita, kuhusu jinsi ya kurusha mabomu ya roketi (RPGs), roketi zinazorushwa kutokea mabegani pamoja na makombora ya kutungua ndege.
Duru hizo zimeongeza kuwa magaidi wakufurishaji wanatazamiwa kuhamishwa ndani ya muda mfupi hadi Mkoa wa Jazira katika mkoa wa mashariki wa Syria wa Dayr al-Zawr na Jangwa la Syria, kaskazini mashariki mwa mji mkuu Damascus, ili kushambulia maeneo ya vikosi vya jeshi la Syria, maeneo muhumu na mikusanyiko ya umma.
Idadi kadhaa ya magaidi wa Daesh waliokamatwa tayari wamekiri kuwa na ushirikiano wa karibu na wanajeshi vamizi wa Marekani walioko katika kambi ya al-Tanf katika mkoa wa Homs wa katikati mwa Syria kwa ajili ya kutekeleza vitendo mbalimbali vya ugaidi na hujuma.
Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Faisal al Mikdad alisisitiza kuwa uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Syria ni kinyume cha sheria.
Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 wakati magaidi wa kimataifa, wakipata himaya ya Saudi Arabia, Marekani na waitifaki wao waliposhambulia nchi hiyo ya Kiarabu kwa lengo la kuupa nguvu zaidi utawala wa Kizayuni wa Israel. Kwa muda mrefu Syria imekuwa kituo cha harakati za kupigania ukombozi wa Palestina.
342/